Thursday, October 16, 2008

Walimu Wagoma Kibaridi


KAMA sheria mpya ya kazi ina mtihani mkubwa wa kwanza tangu ianze kutumika mwaka 2006, basi uamuzi wa jana ndio mtihani mwafaka baada ya walimu katika mikoa mingi nchini, kupuuza amri ya mahakama ya kuzuia mgomo na kutekeleza dhamira yao kwa njia tofauti.

Jumatatu, Jaji William Mandia wa Mahakama ya Kazi alitoa uamuzi wa kuzuia mgomo wa walimu, baada ya kuridhika kuwa mgomo huo ungeathiri sekta nzima ya elimu na hasa wanafunzi ambao wanaendelea na mtihani wa taifa wa kumaliza kidato cha nne. Jaji huyo alitoa amri hiyo baada ya serikali kufungua kesi na kuwasilisha ombi la kuzuia mgomo huo uliopangwa kuanza jana.

"Tumechukizwa sana na kitendo cha serikali kutaka kutuziba midomo kwa kwenda mahakamani. Sasa sisi walimu wa Tarime tunawaomba waje kutufukuza kazi wote," alisema mwenyekiti wa CWT wilayani Tarime, Matinde Magabe.

"Ni aibu kwa serikali kwenda mahakamani eti kuzuia mgomo. Sasa wao waje kufundisha huku vijijini, si wanatudharau sisi."

Naye mwalimu aliyejitambulisha kwa jina la Hassan wa wilayani Tarime alimwambia mwandishi wetu akisema: “Mimi nimekasirika sana kuona serikali inakwenda mahakamani kuweka pingamizi ili tusidai haki yetu. Hivi hawa viongozi kwa kuwa wanaona mambo yao yanawaendea vizuri kutokana na kusomesha watoto wao shule za nje, ndio wanakuwa hawana uchungu na walimu wa Tanzania.”

Walimu hao wanaidai serikali zaidi ya Sh16 bilioni, ikiwa ni sehemu ya Sh23 bilioni ambazo wafanyakazi wanaidai serikali. Limbikizo hilo la fedha za walimu linatokana na fedha za nauli, posho mbalimbali, fedha za uhamisho, huku baadhi ya walimu wakidai kupandishwa madaraja.

Wakati walimu wakianza mgomo huo baridi, chama chao cha taifa jana kilikuwa kikihaha kuwasilisha rufaa yao kwenye Mahakama ya Rufaa kutaka amri hiyo ya Jaji Mandia iondolewe ili waanze mgomo kama ilivyopangwa.

"Tunawasilisha rufaa yetu kesho (leo) na tutasubiri uamuzi iwapo itapita, tutatangaza kuanza mgomo mara moja," alisema mwanasheria wa CWT, Leonard Haule.

"Mgomo wetu ulifuata sheria zote na hivyo ulikuwa halali, lakini mahakama ilizuia kwa muda tu. Walimu lazima waelewe kuwa mgomo haujafutwa, bali umesimamishwa na mahakama. Kwa hiyo rufaa yetu ikishinda, tutaendelea kama ilivyopangwa."

Paulina David kutoka Mwanza anaripoti kuwa, walimu walikuwa wakiimba nyimbo za kutiana nguvu wakati walipokutana kwenye viwanja vya Ghandhi kuanza mgomo.

"Kama sio juhudi zetu walimu... na Kikwete angetoka wapi. Kama siyo juhudi zetu walimu... na majaji wangetoka wapi. Kama siyo juhudi zetu walimu na Maghembe angetoka wapi," ndivyo walivyoimba walimu hao jana.

Walimu hao walikubaliana kuwa wasiende kabisa kazini jana na kwamba leo waende kutia saini tu halafu waondoke bila ya kufanya kazi, lakini Ijumaa wakutane tena kwenye viwanja vya Ghandhi na kujadili mambo yao.

“Tunatoka hapa kwenda nyumbani kulala kesho tunakwenda kusaini kwenye kitabu cha mahudhurio, keshokutwa tunarudi hapa hapa kuendelea na mazungumzo yetu,” alisema mmoja wa walimu

Mwenyekiti wa CWT wa Mwanza, John Kafimbi, alisema kuwa walikataliwa kutumia Ukumbi wa Ghandhi na wamiliki wake waliosema kuwa kutumia ukumbi huo kungemaanisha wamiliki hao kubariki mgomo.

Jijini Dar es salaam, Patricia Kimelemeta anaripoti kuwa walimu walikuwa wakiendesha mgomo baridi baada ya kuripoti kwenye vituo vya vya kazi, lakini wakaamua kutoingia darasani.

Katika baadhi ya shule, walimu hao waliwatangazia wanafunzi wao kuwa hawangeingia madarasani kutokana na sababu zao.

Katika Shule ya Msingi ya Makuburi iliyopo Manispaa ya Kinondoni, walimu hawakuingia madarasani.

“Tumetangaziwa mstarini kuwa walimu hawaingii madarasani kutokana na sababu zao, hivyo basi tumeshindwa kufanya mtihani wa moko na mpaka sasa hatujafundishwa somo lolote na muda wa kuondoka umefika,” alisema mwanafunzi mmoja wa shule hiyo.

Shule nyingine zilizokumbwa na sakata hilo ni Shule ya Msingi Mabibo na Mlimani zilizo Kinondoni wakati kwenye Manispaa ya Ilala ni Shule ya Msingi ya Ulongoni.

Naye Mussa Juma kutoka Tarime anaripoti kuwa zaidi ya walimu 800 walianza mgomo wa kuingia madarasani baada ya uamuzi wa kuridhia mgomo huo kufikiwa jana kwenye Shule ya Msingi ya Turwa.

Walimu hao wanaidai serikali zaidi ya Sh400 milioni.

Akizungumza na Mwananchi baada ya kikao hicho, mwenyekiti wa CWT wilayani Tarime, Matinde Magabe alisema wamekubaliana kuanzia jana kuacha kufundisha.

Mwenyekiti huyo alisema walimu wa wilaya hiyo ya Tarime na wilaya mpya ya Rorya watakuwa wakifika shuleni na kusaini daftari na baadaye kurejea majumbani.

Alisema walimu wa Tarime pekee wanaidai serikali jumla ya Sh236 milioni wakati wa Rorya wakiwa wanadai Sh178 milioni, fedha ambazo ni malimbikizo ya madai mbalimbali.

Mwenyekiti huyo alisema malimbikizo hayo ni pamoja na malipo ya usafiri, likizo, nyongeza za mishahara na malipo mengine ambayo yapo katika mikataba yao ya ajira.

"Pia hapa kuna walimu zaidi ya 500 hawajawahi kupandishwa madaraja hivyo tuna kila sababu ya kuanza mgomo huu," alisema Magabe na kusisitiza kuwa mgomo utaisha pale tu watakapolipwa madai yao yote.

Kutoka Serengeti, Anthony Mayunga anaripoti kuwa walimu katika kata za Issenye, Kisangura, Manchira, Mugumu Mjini, Rung'abure, Machochwe, Ikoma na Kyambahi, waliohojiwa kwa nyakati tofauti, walikiri kuwepo mgomo baridi licha ya serikali kusambaza waraka kuwasihi wasigome.

"Inachofanya serikali ni mchezo wa kuigiza kwa kuwa unaweza kulazimisha punda kwenda mtoni, lakini huwezi kumlazimisha kunywa maji," alisema mwalimu mmoja akimaanisha amri ya Mahakama Kuu kutaka wasigome na uamuzi wao wa kwenda kazini bila ya kufundisha.

Katibu wa CWT wilayani, Wanjala Nyeoja alidai kuwa mgomo baridi unaoendelea ni ishara tosha kuwa walimu wamekata tamaa, wamechoka kuona wanasiasa wananeemeka kwa njia za propogandaa, wakati afisa elimu wilaya, Ishengoma Kyaruzi alidai kuwa alikuwa anafuatilia mashuleni kuona hali halisi ilivyo.

Naye Burhani Yakub wa Tanga anaripoti kuwa walimu wengi kwenye wilaya za mkoa huo walitumia siku ya jana kupiga soga badala ya kuingia darasani, ikiwa ni njia mojawapo ya kugoma.

Wilayani Handeni, Mwananchi imefahamishwa kuwa walimu wa baadhi ya shule zilizopo katika mji wa Chanika walitumia siku ya jana kupiga gumzo wakati wa masomo.

Wakizungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa majina yao wala shule wanazofundisha, walimu hao walisema wataendelea na mgomo baridi hadi watakapopata maelekezo mengine kwa kuwa hawana tena ari ya kufanya kazi.

Wilayani Pangani, baadhi ya walimu walisema hawako tayari kufundisha kwa sasa licha ya amri ya mahakama na kwamba wanachotaka ni serikali kuwalipa madai yao badala ya kutafuta njia za kuwatisha kwa kutumia sheria.

Kutoka Sumbawanga, Oscar Simon anaripoti kuwa walimu wilayani Mpanda waliwarejesha majumbani wanafunzi na baadaye walimu kuondoka katika vituo vyao vya kazi, wakiwaacha walimu wakuu pekee.

Mmoja wa walimu ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, alisema kwa njia ya simu kuwa wameanza mgomo huo kama kawaida na kamwe hawataweza kutii agizo la mahakama na viongozi wao la kuacha mgomo

kwani wanaamini kuwa walimu wenyewe ndio wanapaswa kuamka na kudai haki yao.

"Tumefika shuleni kama kawaida, na baadaye tukakubaliana tunaendesha mgomo wetu kama tulivyoazimia. Hivyo tukatawanyika kwenda kuendelea na shughuli nyingine. Hii serikali si ya kucheka nayo... wao ndio vinara wa ufisadi huko juu wanataka kutukandamiza sisi kila siku kwa kutumia mgongo wa mahakama," alisema mwalimu huyo.

Mwl. Juma Kablanketi wa Shule ya Msingi Kashato mjini Mpanda alisema kuwa kimsingi wamekubaliana watakutana kesho kutathimini mgomo wao kama unaendelea au wanarejea kazini kuanzia Jumatatu ijayo.

Kutoka Kibaha, Julieth Ngarabali anaripoti kuwa vikao vya dharura vya viongozi wa CWT wa mkoa wa Pani vilipangwa kufanyika juzi maeneo ya Ruvu, Mlandizi, Kisarawe, Chalinze na Mkuranga na vilikuwa viongozwe na Mwenyekiti Kelvin Mahundi na katibu wake.

Lakini wajumbe waliojitokeza waliwaeleza viongozi hao kuwa hawaelewi kufika kwake kulikuwa na malengo gani na kushangazwa na uamuzi wa Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi, wa kuwataka warejee makazini.

CWT Pwani ilitoa tamko la kuridhia kutoanza mgomo kwa sharti kwamba rufaa ikatwe.

Mwenyekiti Mahumbi alisema pamoja na chama hicho kutoa tamko hilo, hana uhakika kama walimu wote watarejea kazini kwa ari ya kutekeleza majukumu yao kweli ama watakuwa wanazuga tu huko mashuleni.

Uchunguzi wa Mwananchi kwenye shule mbili za sekondari za shirika la elimu Kibaha, shule ya msingi na sekondari ya Nyumbu, Kibaha, Mwendapole, Muungano, Mkoani na Mailimoja, ulionyesha kuwa walimu wengi walikuwa wakiendelea na shughuli zao.

Jijini Dar es salaam, ambako wanachama wa CWT walizua tafrani kubwa wakati viongozi wao walipowataarifu kuwa mgomo umezuiwa, jana walionekana kama wamepungua hasira na shule nyingi zilionekana kuendelea na shughuli za elimu kama kawaida.

Ummy Muya anaripoti kuwa hali ilikuwa shwari katika shule mbalimbali za serikali, zikiwemo Forodhani na Kisutu zilizo katikati ya jiji.

"Hatuwezi kuja maeneo ya kazi na kukaa bila kufanya kazi kwa kuwa kufanya hivyo ni kuwaumiza wanafunzi na sisi mdeni wetu ni serikali kupitia wizara ya elimu," alisema mmoja kwa sharti la kutotajwa jina, lakini akageuka na kusema: "Viongozi wengi wanaisahau sekta ya elimu kwa kuwa watoto wao wanasoma nje ya nchi. Na hata kama wanasoma nchini ni katika shule za kimataifa."

Naye Furaha Kijingo anaripoti kuwa katika Shule ya Msingi Makumbusho na Victoria walimu walikuwa wakiendelea kufundisha kama kawaida.

"Hapa shuleni kwetu hali ni shwari na siwezi kuzungumza lolote kwani maelezo yote yapo kwa mkurugenzi wa manispaa," alisema mwalimu mkuu wa shule hiyo.

No comments: