Friday, November 28, 2008

MAUAJI ya kinyama ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) huenda sasa yameingia katika jiji la Dar es Salaam, kufuatia kukamatwa watu wawili wanaotuhumiwa kufanya jaribio la kuwaiba watoto wawili ndugu ambao ni albino, Irene Stanclaus (10) na mdogo wake, Gerald Stanclaus ,4, (picha kubwa ukurasa wa mbele) wakazi wa Kipawa, Dar es Salaam.

Watoto Maalbino Gerald Stanslaus (4), kushoto, na Irene Stanslaus (10) wakiwa nyumbani kwao na Mlezi wao Bw. Alex Lwetabira baada ya kutoka Kituo cha Polisi Ukonga Sitaki Shari, Dar es Salaam amabako walikwenda kutoa ushahidi baada ya kunusurika kutekwa jana na watu wawili waliokamatwa na wananchi wakitaka kufanya kitendo hicho.

Chanzo chetu kutoka eneo la tukio kililiarifu Majira jana mchana kutokea kwa tukio hilo ambapo watu hao waliojulikana kwa majina mojamoja, Bw. Juma na Bw. Thobias walikamatwa baada ya wasamaria wema kugundua njama hizo jana wakiwa tayari wamejiandaa kuwateka watoto hao na kuwapeleka kusikojulikana kwa nia ya kuwauza.

Mama wa watoto hao, Bi. Evodia Stanclaus (34) akizungumzia mkasa huo wa kusikitisha aliliambia gazeti hili kuwa alipata taarifa za watoto wake 'kuwindwa' na watu wawili waliokuwa wakirandaranda katika maeneo ya nyumbani kwake wakijifanya kutafuta simu ya mkononi yenye kamera.

Alisema alipata taarifa hiyo saa 5 asubuhi kuwa kuna vijana hao wanataka kuwaiba watoto wake na njama hizo ziligunduliwa na majirani ambao waliwasikia vijana wakisuka mipango ya namna watakavyoweza kuwapata majirani watakaowatoa watoto hao nje ili waweze kuondoka nao.

Mama huyo aliongeza kuwa vijana hao waligawana majukumu mmoja alikwenda duka la karibu na nyumbani hapo na kununua soda na kuomba apewe kiti cha kuketi na mwingine alifika nyumbani kwake akijifanya kutafuta simu ya kamera.

Alisimuliza zaidi kuwa wakati wakitafuta njia za kuwatoa watoto hao nje ili wawateke majirani walishituka hasa baada ya kubaini kuwa vijana hao ni wageni kwenye mitaa hiyo ndipo walipowahoji na kutaka wajue wanakotoka lakini kila walipobanwa walitaja kutoka maeneo tofauti hivyo wakawaweka chini ya ulinzi.

Kwa mujibu wa majirani hao, baada ya kuwekwa nguvuni huku umati wa watu ukilizingira zaidi eneo hilo, mmoja wa vijana hao alikiri kuwa walitumwa na tajiri mmoja ambaye alikataa kumtaja na ilikuwa wawachukue albino hao hadi Njiapanda ya Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere ili wakodishe gari kuwapeleka watoto hao walipotakiwa kupelekwa.

Mjumbe wa Nyumba Kumi jirani na nyumbani kwa watoto hao, Bibi. Anna Mbise alikiri kumuona mmoja wa vijana hao ambaye alifika dukani kwake kununua soda na wakati akinywa aliomuona kijana mwingine ambayo baada ya kuona wamestukiwa mpango wao 'alitokomea' kabla ya kukutwa akiwa amejifanya mgonjwa kwa kuingia katika zahanati moja ya jirani.

Wananchi hao walipombana waligundua kijana huyo hakuwa mkweli kwani aliwatajia jina ambalo ni tofauti na alililokuwa amejiandikisha kwenye zahanati hiyo hali iliyowafanya wananchi hao kuzidi kubaini vijana hao hawakuwa watu wema.

Mkuu wa Wilaya ya Kipolisi ya Ukonga, Bibi. Maleta Komba alipoulizwa kushikiliwa kwa watu hao hakukiri wala kukanusha bali alisema msemaji wa Polisi ni Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Bw. Suleiman Kova.

Hata hivyo baba mlezi wa watoto hao, Bw. Alex Rwetabila akizungumza nyumbani kwake Kipawa, alieleza kusikitishwa na kitendo hicho na kuhofu usalama wa watoto hao kiasi cha kulazimika kuwafungia ndani muda wote wakiwa chini ya ulinzi mkali.

Naye mtoto Irene aliyenusurika kutekwa akizungumza mara baada ya kutoka polisi kuhojiwa alikiri kumuona kijana mmoja aliyefika nyumbani kwao akijifanya anauliza sehemu anakoweza kununua simu ya kamera kwani alipata taarifa kuwa nyumbani hapo kuna simu ya kamera iliyokuwa ikiuzwa na mama mzazi wa mtoto huyo.

"Nilimuona mtu huyo alipokuja nyumbani kuuliza masuala ya simu, baadaye nikasikia alikuwa akitaka kututeka. ndipo tukachukuliwa mimi na mdogo wangu kwenda kutoa maelezo polisi," alisema Irene ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne kwenye Shule ya Msingi Minazi Mirefu, Ukonga, Dar es Salaam.

No comments: