Thursday, November 20, 2008

Mtoto wa Binadamu Alelewa na Nyani Miaka 5 Porini

WATANZANIA wameombwa kujitokeza kumsaidia kielimu mtoto Bahati Baraka Rose (11) ambaye anadaiwa kulelewa na nyani baada ya kutupwa porini akiwa mchanga wilayani Bukombe, Shinyanga.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kimanga, Tabata, Bw. Pastory Kyombya, alisema mtoto huyo kwa sasa analelewa na Bibi Rose Mbwambo wa Kimanga.

Alisema Bibi Mbwambo alikabidhiwa mtoto huyo na Serikali wilayani Bukombe baada ya kufuata taratibu zote za kiserikali.

Alisema Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukombe, Bw. Richard Nhende, ndiye aliyemkabidhi Bibi Mbwambo mtoto huyo ili amlee baada ya kumwomba.

Bw. Kyombya alisema mtoto huyo anaomba kupelekwa shule kama anavyoshuhudia wenzake wakienda shule na kuwaomba wasamaria wema wajitokeze kumsaidia ili aanze shule mwakani.

Naye Bibi Mbwambo alisema alimchukua mtoto huyo Agosti mwaka huu akiwa kwenye biashara zake Bukombe.

"Nilikuwa nimepanga kwenye nyumba ya kulala wageni ya Neema, nikiwa na wenzangu, mama mmoja (hakumtaja jina) ambaye alikuwa akitupikia chakula alitujia na kutueleza matatizo aliyonayo mtoto Baraka.

"Nilimwonea huruma sana Baraka, baada ya mama huyo kutuelezea historia yake nzima na kwamba hana ndugu na maisha yake ni ya kutangatanga na kututaka tumsaidie," alisema.

Alisema yeye binafsi aliingiwa na huruma ndipo alipofuata taratibu zote za kumchukua mtoto huyo na kuja naye Dar es Salaam kumlea.

Bibi Mbwambo alisema atamtunza mtoto huyo kama anavyotunza watoto wake ila aliomba wasamaria wema kujitokeza kumsaidia ili aanze masomo mwakani ikiwezekana shule ya bweni.

Alisema mtoto huyo alilelewa na nyani miaka kadhaa porini kabla ya kuchukuliwa tena na binadamu baada ya nyani huyo mlezi kuuawa kwa risasi.

Bibi Mbwambo alisema inadaiwa mtoto huyo aliokotwa na nyani akiwa kwenye mfuko wa 'rambo' akiwa mchanga na kumlea kwa miaka mitano.

"Askari wa wanyamapori wa Ushirombo, Bukombe, ndio waliofanikisha kupatikana kwa mtoto huyo baada ya siku moja kumwona nyani akimnyonyesha.

"Hata hivyo, inadaiwa askari hao walipata shida kumchukua mtoto huyo baada ya nyani mlezi kukimbia naye mara zote kila alipokuwa akiwaona, hivyo kuchukua muda mrefu kumpata," alisema.

Alisema mtoto huyo aliendelea kulelewa na nyani huyo hadi alipofikisha umri wa miaka mitano na baadaye askari hao kumvamia tena ili kumnyang'anya mtoto huyo na kusababisha vurugu kubwa kati yao na nyani mlezi.

Bibi Mbwambo alisema katika vurugu hizo, askari walimfyatulia risasi nyani huyo na kumuua huku risasi moja ikimpata mtoto huyo kwenye kidole cha mguu wa kushoto.

Alisema askari hao walimchukua mtoto huyo na kumpeleka katika hospitali ya Bukombe ambako aliendelea kulelewa hospitalini hapo.

Bibi Mbwambo alisema watu mbalimbali walikuwa wakimchukua mtoto huyo na kumlea na walioshindwa walikuwa wakimrudisha hospitalini hapo, lakini msamaria mwema alimchukua, lakini mtoto huyo alimtoroka na kuingia mitaani na kuishi maisha ya shida.

Alisema Baraka alikwishazoea kuishi maisha ya porini, akiparamia miti na kusababisha wasamaria wema waliokuwa wakimlea kulazimika kumfunga minyororo ili asitoroke.

No comments: