Friday, November 7, 2008

Pinda Akabidhiwa 'Kitanzi' Cha Makamba

SHINIKIZO la wabunge wa CCM la kutaka kung’olewa kwa Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusuph Makamba, limechukua sura mpya baada ya wabunge wa chama hicho kuwasilisha hoja hiyo kwa Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM, Bw. Mizengo Pinda, kwa madai kuwa anakigawa chama. 

Hatua hiyo ilijitokeza juzi jioni katika kikao cha wabunge hao ambacho kilipangwa kufanyika saa 10 jioni, lakini kikachelewa kutokana na mgongano wa wabunge hao ambao baadhi ya hoja zilizokuwa mezani lizipingwa. 

Kwa mujibu wa chanzo cha habari cha kuaminika kutoka ndani ya chama hicho, katika mambo yaliyozungumzwa ni hoja ya kutaka kung’olewa kwa Bw. Makamba katika kiti hicho, kwani amekuwa akifanya mambo yanayowagawa wana CCM. 

“Hoja hii tumeifikisha kwa Mwenyekiti wetu ambaye naye anasema hawezi kutoa jibu, bali atalifikisha kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, ambaye ni Rais Jakaya Kikwete,” kilisema chanzo hicho. 

Sababu za kutaka aachie nafasi hiyo ni madai ya kupokea wanachama kutoka vyama vya upinzani na kuwapa madaraka makubwa bila uchunguzi wa kutosha. 

“Mbali na hili, jingine ni la Tarime ambako alipeleka watu wasiokuwa na uzoefu wa kutosha katika masuala ya kampeni, lakini kubwa zaidi alifikia kwa mwanachama mmoja kitendo kilichowakera wana CCM wengine na kwa kufanya hivyo, ni kuwagawa wanachama,” kilisema chanzo cha habari. 

Tuhuma nyingine ya Bw. Makamba ni kuwachonganisha wabunge hao na wananchi kwa kile alichokitangaza kuwa hawaendi majimboni mwao. 

Suala lingine lililoibuka ndani ya mkutano huo, ni wabunge hao kupendekeza baadhi ya mawaziri wenye nyadhifa kubwa ndani ya chama, kuchagua suala moja la ama kuachia ngazi ya uwaziri au nafasi ya uongozi katika chama. 

“Wapo hawa mawaziri hawana muda sasa wa kukitumikia chama vizuri, hivyo ifike mahali wachague kitu kimoja, kwani lengo letu sasa ni kukijenga chama na si kuendelea kukibomoa,” kilisema chanzo kingine cha habari. 

Kitu kingine kilichoibuka ni wabunge wa viti maalumu kuingilia wenzao katika majimbo yao, hali inayoleta picha mbaya na kuonesha tamaa ya madaraka. 

Masuala haya mazito yalijitokeza wakati wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wanatarajia kuanza mkutano wao mjini hapa kesho, ambao unatarajiwa kuwa na ajenda nzito. 

Akizungumza juzi na gazetihili, Bw. Makamba alikanusha kuwapo kwa mpango huo, akisema ni hisia za mtu mmoja na kama zingekuwa za wabunge wa CCM angeshapata taarifa. 

Alitaka mawazo hayo yachukuliwe kama masuala ya mitaani na kwamba vikao maalumu ndivyo vinavyoweza kuamua hatima yake. 

Baadhi ya viongozi waliotoka Upinzani na kupewa nyadhifa ndani ya CCM ni Bw. Tambwe Hiza aliyekuwa CUF, Bw. Salum Msabah kutoka CUF na wengineo.

No comments: