Sunday, September 28, 2008

Si Kila Kiongozi ni Fisadi - JK


RAIS Jakaya Mrisho Kikwete amesema si kila kiongozi wala kila mtumishi wa umma barani Afrika ni mla rushwa ingawa amekiri kwa kiasi fulani tatizo hilo bado lipo barani humo. 

Rais alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu maswali baada ya kumaliza hotuba yake kwenye mkutano na wajumbe wa taasisi ya Foreign Policy Brain Trust ambayo ni ya wabunge wenye asili ya Afrika mjini Washington. 

"Tusijiweke katika hali ya kutengeneza mazingira ya kwamba kila jambo linaloendelea katika Afrika ni rushwa tu," alisema Rais Kikwete. 

Aliongeza kuwa: "Hatukatai kuwa ipo rushwa katika Afrika. Tunachosema ni kwamba jambo hilo linatiwa chumvi nyingi kupita kiasi". 

Kuhusu Tanzania, Rais Kikwete alisema kuwa Serikali yake inapambana kwa dhati na changamoto hiyo ya rushwa kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya Tanzania. 

"Moja ya dalili za Serikali inayokula rushwa ni kushuka kwa mapato ya Serikali au Serikali kushindwa kukusanya mapato. Mapato yetu (Tanzania) yamekuwa yakiongezeka kila mwaka tokea tulipoingia madarakani," alisema Rais Kikwete na kushangiliwa.

No comments: