Monday, November 3, 2008

Wizi wa EPA: Nitachambua Faili Moja Baada ya Jingine Asema DPP

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) amesema atachambua kwa makini "faili moja baada ya jingine" baada ya kukabidhiwa rasmi mafaili ya wezi wa fedha kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na hivyo kufanya uwezekano wa watuhumiwa hao kufikishwa mahakamani katika siku chache zijazo kuwa mdogo.

Kuwasilishwa kwa mafaili ya mafisadi hao walioshindwa kurejesha Sh64 bilioni kati ya Sh133 bilioni zilizochotwa kwenye akaunti hiyo, kunafanya mzigo huo sasa uelemee kwa DPP, Eliezer Felesh ambaye ofisi yake ilikabidhiwa mafaili hayo jana na Mwanasheia Mkuu wa Serikali.

Hatua hiyo imekuja wakati hali ikiwa tete kutokana na wananchi wa kada mbalimbali, wakiwemo wabunge na wasomi kutaka wezi wote wa fedha hizo wafikishwe mahakamani tofauti na agizo la Rais Jakaya Kikwete kuwa wale ambao wangeshindwa kurejesha fedha hizo kabla ya Oktoba 31 tu ndio wafikishwe mahakamani.

Kwa mujibu wa duru mbalimbali za kiserikali, kazi kubwa iliyopo sasa inafanywa na Kurugenzi ya Upelelezi ya Makosa ya Jinai ambayo imeelezwa kuwa tayari imewaweka chini ya ulinzi watuhumiwa ikisubiri kuwafikisha mahakamani wakati wowote kwa maelekezo ya DPP, ambaye hana budi kujiridhisha kwanza dhidi ya tuhuma hizo za ufisadi kabla ya kuruhusu sheria ichukue mkondo wake.

Wakati Wizara ya Sheria na Katiba ikitoa taarifa rasmi ya kuwasilishwa majalada yote ya watuhumiwa kwa DPP, Feleshi alilithibitishia gazeti hili jana kwamba tayari ameanza kuyachambua majalada hayo.

"Kila jalada linalokuja lazima nilisome, nilipitie kwa umakini... ndiyo utaratibu huo, hatupindishi sheria, lakini hadi sasa (jana) siko katika nafasi ya kueleza idadi ya majalada ambayo yamekuja," alifafanua DPP Feleshi.

Feleshi, ambaye ni mmoja wa watendaji serikalini wasio na urasimu wa kutoa habari, alisema hakuna mtu atapona au kuonewa katika mchakato huo.

"Hakuna namna ya mtu kuweza kupona au kuonewa, lazima nifanye Legal Analysis (uchambuzi wa kisheria) kwanza, cha msingi usiulize majalada mangapi, niulize afya yangu tu, niombe uzima tu, kila kitu utaona kitakavyokwenda," alisema DPP Feleshi.

Feleshi alisisitiza kuwa jambo kubwa na la msingi analoomba ni kuwa na afya njema kwani ana uhakika wa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria bila kupindisha.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, aliliambia gazeti hili kwamba polisi sasa inamsikiliza mkuu huyo wa mashitaka.

Kamishna Manumba alisema DPP ndiyo kiongozi wa kazi hiyo atakolosema polisi itafanya kwa mujibu wa taratibu.

"Hivi sasa kiongozi wetu ni DPP, atakachosema polisi tutafanya, kazi hii inahusisha taasisi nyingi hivyo mkurugenzi wa mashitaka ndiyo kiongozi wetu," alisisitiza Kamishna Manumba.

Wakati vigogo hao kutoka ofisi ya DPP na Polisi wakitoa misimamo hiyo, taarifa nyingine kutoka wizara hiyo ya sheria na Katiba iliyotolewa jana mchana na msemaji wake, Omega Ngole, ilisema timu ya rais imetimiza maelekezo yote ya mkuu wa nchi.

Timu ilisema kiasi cha fedha cha Sh69.3 bilioni alichotaja rais hakijaongezeka hadi kufikia Oktoba 31 na majalada yote ya kesi yameshawasilishwa kwa DPP.

"Timu inapenda kuarifu umma kuwa maelekezo yote mawili yametekelezwa. Kiasi cha fedha kilichorejeshwa hadi mwishoni mwa Ijumaa (Oktoba 31,2008) ni kilekile kilichotajwa na Mheshimiwa Rais, yaani sh 69.3 bilioni. Aidha, majalada ya kesi yamewasilishwa kwa DPP kwa ajili ya kuyafanyia kazi kama ilivyoelekezwa," alifafanua Ngole.

Akihutubia taifa Ijumaa, Rais Kikwete alisema ameagiza timu yake kwamba wamiliki wa makampuni 13 ambayo yalichota sh 90.3 bilioni na kisha yakashindwa kurejesha fedha zilizobaki, majalada yao yapelekwe kwa DPP ambaye kikatiba ndiye mwenye mamlaka ya kuandaa taratibu za kufungua mashitaka.

Hata hivyo, kauli hiyo bado ilionekana kupingwa na baadhi ya Watanzania wa kada mbalimbali ambao walisema wana imani na wanamuunga mkono Rais Kikwete, lakini wakataka mashitaka yasiwe kwa baadhi ya watuhumiwa, bali kwa wote walioiba.

Lakini, duru nyingine zinadai kuwa uamuzi huo huenda ukawa ni mbinu ya kuwatega mafisadi hao ili warejeshe fedha wote ili kiwe kidhibiti cha kuburuza nacho mahakamani kwa urahisi.

Ufisadi wa EPA ulibainika katika hesabu za BoT za mwaka 2005/06, baada ya ukaguzi wa kampuni ya Deloitte&Touche ya Afrika Kusini, ambayo ilisitishwa ghafla na Benki Kuu (BoT) kufanya kazi bila sababu za msingi baada ya kubaini Sh40 bilioni zilizochotwa na kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.

Hata hivyo, mwaka jana serikali ilimwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutafuta kampuni ya kimataifa ya kufanya tena ukaguzi.

Ofisi ya CAG iliteua kampuni ya kimataifa ya Ernst&Young, ambayo ilibaini ufisadi huo wa Sh133 bilioni, ambazo zilichotwa na makampuni 22.

Makampuni 13 yalijichotea sh 90.3 bilioni, ni pamoja na Bencon International LTD of Tanzania, Vb & Associates LTD of Tanzania, Bina Resorts LTD of Tanzania, Venus Hotel LTD of Tanzania, Njake Hotel &Tours LTD, Maltan Mining LTD ya Tanzania.

Mengine ni Money Planners & Consultants, Bora Hotels & Apartment LTD, B.V Holdings LTD, Ndovu Soaps LTD, Navy Cut Tobacco (T) LTD, Changanyikeni Residential Complex LTD na Kagoda Agriculture LTD.

Kwa upande wa makampuni tisa yaliyochota Sh42.6 bilioni yanasubiri uchunguzi zaidi unaofanywa kwa kuhusishwa serikali za nchi nyingine baada ya hatua za awali kutotoa majibu mazuri.

Makampuni yaliyo kwenye sakata hilo ni G&T International LTD, Excellent Services LTD, Mibale Farm, Liquidity Service LTD, Clayton Marketing LTD, M/S Rashtas (T) LTD, Malegesi Law Chambers (Advocates), Kiloma and Brothers na KARNEL LtD.

Kumbukumbu ya makampuni mengine mawili- Rashtas (T) na G&T International LTD, pamoja na nyaraka za usajili kwa Msajili wa Majina ya Makampuni na Biashara (BRELA), hazikuweza kupatikana.

Kufikia mwaka 1999 deni katika EPA lilifikia dola 623 milioni, ambazo kati ya hizo dola 325 milioni zilikuwa ni deni la msingi na dola 298 ni riba na baadaye deni likaongezeka hadi kufikia dola 677 milioni.

Hata hivyo, chini ya Mpango wa Kununua Madeni (Debt Buy Back Scheme) wa mwaka 1994 kati ya serikali na Benki ya Dunia (WB), waliokuwa wanaidai BoT waliombwa wakubali kulipwa sehemu tu ya fedha wanazodai. Wapo waliokubali na wengine kukataa na kuongeza hadi mwaka 2004 taarifa zinaonyesha jumla ya dola 228 zililipwa chini ya mpango huo.

EPA ni akaunti ya madeni ambayo ilitumika wakati wa Mfumo wa Ujamaa, ambayo akaunti yake ilikuwa katika iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) chini ya usimamizi wa BoT.

Mwaka 1985, EPA ilihamishiwa moja kwa moja BoT, na ndipo mwaka juzi kulipoibuka utata wa tuhuma za ufisadi katika akaunti hiyo kwa mahesabu ya mwaka 2005/06, ambayo utata huo ulisababisha Ernst&Young kufanya ukaguzi kuanzia Septemba sita na kukabidhi ripoti yake kwa CAG mapema Desemba mwaka jana

No comments: