Friday, November 28, 2008

MAUAJI ya kinyama ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) huenda sasa yameingia katika jiji la Dar es Salaam, kufuatia kukamatwa watu wawili wanaotuhumiwa kufanya jaribio la kuwaiba watoto wawili ndugu ambao ni albino, Irene Stanclaus (10) na mdogo wake, Gerald Stanclaus ,4, (picha kubwa ukurasa wa mbele) wakazi wa Kipawa, Dar es Salaam.

Watoto Maalbino Gerald Stanslaus (4), kushoto, na Irene Stanslaus (10) wakiwa nyumbani kwao na Mlezi wao Bw. Alex Lwetabira baada ya kutoka Kituo cha Polisi Ukonga Sitaki Shari, Dar es Salaam amabako walikwenda kutoa ushahidi baada ya kunusurika kutekwa jana na watu wawili waliokamatwa na wananchi wakitaka kufanya kitendo hicho.

Chanzo chetu kutoka eneo la tukio kililiarifu Majira jana mchana kutokea kwa tukio hilo ambapo watu hao waliojulikana kwa majina mojamoja, Bw. Juma na Bw. Thobias walikamatwa baada ya wasamaria wema kugundua njama hizo jana wakiwa tayari wamejiandaa kuwateka watoto hao na kuwapeleka kusikojulikana kwa nia ya kuwauza.

Mama wa watoto hao, Bi. Evodia Stanclaus (34) akizungumzia mkasa huo wa kusikitisha aliliambia gazeti hili kuwa alipata taarifa za watoto wake 'kuwindwa' na watu wawili waliokuwa wakirandaranda katika maeneo ya nyumbani kwake wakijifanya kutafuta simu ya mkononi yenye kamera.

Alisema alipata taarifa hiyo saa 5 asubuhi kuwa kuna vijana hao wanataka kuwaiba watoto wake na njama hizo ziligunduliwa na majirani ambao waliwasikia vijana wakisuka mipango ya namna watakavyoweza kuwapata majirani watakaowatoa watoto hao nje ili waweze kuondoka nao.

Mama huyo aliongeza kuwa vijana hao waligawana majukumu mmoja alikwenda duka la karibu na nyumbani hapo na kununua soda na kuomba apewe kiti cha kuketi na mwingine alifika nyumbani kwake akijifanya kutafuta simu ya kamera.

Alisimuliza zaidi kuwa wakati wakitafuta njia za kuwatoa watoto hao nje ili wawateke majirani walishituka hasa baada ya kubaini kuwa vijana hao ni wageni kwenye mitaa hiyo ndipo walipowahoji na kutaka wajue wanakotoka lakini kila walipobanwa walitaja kutoka maeneo tofauti hivyo wakawaweka chini ya ulinzi.

Kwa mujibu wa majirani hao, baada ya kuwekwa nguvuni huku umati wa watu ukilizingira zaidi eneo hilo, mmoja wa vijana hao alikiri kuwa walitumwa na tajiri mmoja ambaye alikataa kumtaja na ilikuwa wawachukue albino hao hadi Njiapanda ya Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere ili wakodishe gari kuwapeleka watoto hao walipotakiwa kupelekwa.

Mjumbe wa Nyumba Kumi jirani na nyumbani kwa watoto hao, Bibi. Anna Mbise alikiri kumuona mmoja wa vijana hao ambaye alifika dukani kwake kununua soda na wakati akinywa aliomuona kijana mwingine ambayo baada ya kuona wamestukiwa mpango wao 'alitokomea' kabla ya kukutwa akiwa amejifanya mgonjwa kwa kuingia katika zahanati moja ya jirani.

Wananchi hao walipombana waligundua kijana huyo hakuwa mkweli kwani aliwatajia jina ambalo ni tofauti na alililokuwa amejiandikisha kwenye zahanati hiyo hali iliyowafanya wananchi hao kuzidi kubaini vijana hao hawakuwa watu wema.

Mkuu wa Wilaya ya Kipolisi ya Ukonga, Bibi. Maleta Komba alipoulizwa kushikiliwa kwa watu hao hakukiri wala kukanusha bali alisema msemaji wa Polisi ni Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Bw. Suleiman Kova.

Hata hivyo baba mlezi wa watoto hao, Bw. Alex Rwetabila akizungumza nyumbani kwake Kipawa, alieleza kusikitishwa na kitendo hicho na kuhofu usalama wa watoto hao kiasi cha kulazimika kuwafungia ndani muda wote wakiwa chini ya ulinzi mkali.

Naye mtoto Irene aliyenusurika kutekwa akizungumza mara baada ya kutoka polisi kuhojiwa alikiri kumuona kijana mmoja aliyefika nyumbani kwao akijifanya anauliza sehemu anakoweza kununua simu ya kamera kwani alipata taarifa kuwa nyumbani hapo kuna simu ya kamera iliyokuwa ikiuzwa na mama mzazi wa mtoto huyo.

"Nilimuona mtu huyo alipokuja nyumbani kuuliza masuala ya simu, baadaye nikasikia alikuwa akitaka kututeka. ndipo tukachukuliwa mimi na mdogo wangu kwenda kutoa maelezo polisi," alisema Irene ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nne kwenye Shule ya Msingi Minazi Mirefu, Ukonga, Dar es Salaam.

Friday, November 21, 2008

...Mahakimu Washitaki kwa IGP


MAHAKIMU wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambao hivi karibuni waliripotiwa kulazimika kuomba kuhakikishiwa usalama wao kwa viongozi wa Idara ya Mahakama nchini kutokana na kutishwa na baadhi ya vigogo wa EPA ambao kesi zao zimefunguliwa mahakamani hapo. 

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es salaam jana, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema alithibituisha mahakimu hao kulalamika na jeshi lake limekwishayapokea malalamiko hayo na kuahidi kuyafanyia kazi. 

IGP Mwema alisema, bila kuwataja mahakimu waliolalamika, vitisho hivyo vilianza dhidi ya mahakimu na waendesha mashitaka wa kesi hizo mara tu baada ya washitakiwa mbalimbali kuanza kusimamishwa kortinini hapo. 

"Ni kweli tumepokea malalamiko kutoka kwa mahakakimu na waendesha mashitaka wa kesi za EPA na kwamba tunayafanyia kazi ila tumewahakikishia usalama wao," alisema. 

Aliongeza kuwa mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusika na utoaji wa vitisho hivyo kwa mahakimu na waendesha mashitaka hao. 

Akizungumzia juu ya watuhumiwa wengine wa sakata hilo wanaotarajiwa kufikishwa mahakamani alisema suala hilo lipo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) ambaye amekabidhhiwa ripoti ya uchunguzi juu ya suala hilo. 

Alisema kuwa wao wakiwa Jeshi la Polisi wataendelea kutoa ushirikiano unaohitajika juu ya uendeshaji wa kesi hizo pale watakapohitajika. 

"Sisi tukiwa Jeshi la Polisi tuliteuliwa katika Tume ya Uchunguzi na ripoti tayari ipo kwa DPP, hivyo kama kuna lingine linalohitajika kuhusu hili, tutaendelea kutoa ushirikiano wetu," alisema IGP alipokuwa akijibu swali kuhusu suala hilo la kashifa ya EPA. 

IGP Mwema ni mmoja wa wajumbe katika Timu Maalum iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete ambayo ilipwa jukumu la kuipitia ripoti ya wakaguzi wa Ernst and Young na kutoa mapendekezo yao juu ya namna ya kuwachukulia hatua washitakiwa waliohusika na ufisadi kwenye akaunti ya EPA. 

Wajumbe wengine kwenye kamati hiyo ni Mwanasheria Mkuu, Bw. Johnson Mwanyika ambaye pia ni Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rsuhwa (TAKUKURU), Dkt. Edward Hosea.

Thursday, November 20, 2008

Wanafunzi wa chuo cha IFM wamevamia wizara ya fedha na uchumi


Wanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo cha usimamizi wa fedha ifm wamevamia wizara ya fedha na uchumi wakipinga kiasi kidogo cha fedha kilichotolewa na serikali kwa ajili ya chakula na malazi baada ya kutolipwa kwa takribani miezi miwili. 

Wakiwa wamesimama katika lango kuu la kuingilia katika ofisi za wizara hiyo wanafunzi hao wamedai kuwa kiasi cha shilingi millioni 1 kilichotolewa na wizara hiyo kwa kila mwanafunzi badala ya million 1 na laki 3 hakikikidhi gharama za maisha kutokana na wafunzi wengi kuwa na madeni yaliyotokana na kucheleweshwa kwa malipo na wizara hiyo. 

Aidha ITV ilimtafuta msemaji wa wizara ya fedha na uchumi ili kuzungumzia tatizo hilo bila mafanikio na baadhi ya wafanyakazi waliokwepo katika jengo hilo walidai kuwa yuko katika mkutano.

*Source ITV Medeia*

Tanesco na Dowans

Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, imeshtukia mchezo mchafu uliosukwa na Bodi iliyopita ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), wa kupitisha uamuzi wa ununuzi wa mitambo ya kuzalisha umeme ya Dowans. 

Kulingana na chanzo chetu cha habari, Bodi hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Balozi Fulgence Kazaura, Iliridhia Tanesco kununua mitambo ya Dowans. 

Chanzo hicho kilisema hatua hiyo ilifikiwa na bodi kwa kigezo kimoja cha kwamba, mitambo hiyo ni mipya ilhali imefanyakazi kwa zaidi ya mwaka mmoja tangu kuingizwa nchini. 

Kutokana na hatua hiyo, Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini katika wiki ya mwisho wa mkutano wa Bunge wa 13 mjini Dodoma, ilimwita Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, na kumuonya dhidi ya uamuzi huo. 

``Tulimuonya kuwa kuchukua uamuzi huo ni ukiukaji na dharau dhidi ya agizo la Bunge...ni mwendelezo wa maslahi binafsi ya watendaji waandamizi wa Tanesco kwenye Dowans, kilisema chanzo chetu na kuongeza: 

``Hata Kamati Teule ya Bunge ya Kuchunguza Mchakato wa Ushindi wa Zabuni ya Kuzalisha Umeme wa Dharura iliyotolewa kwa Richmond, iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe ilibainisha haya. 

Katika taarifa ya Kamati ya Mwakyembe, inaonyesha kuna baadhi ya watendaji waandamizi wa Tanesco walishinikiza ushindi wa zabuni hiyo na baadaye kuacha kazi na kujiunga na Kampuni ya Richmond Development na sasa Dowans. 

Taarifa kutoka ndani ya kikao cha kamati na Waziri Ngeleja zinaeleza kuwa, mbunge mmoja (jina tunalo), alifikia hatua ya kumweleza iwapo uamuzi huo utachukuliwa itakuwa imethibitisha hisia zilizoko mitaani kuwa mtandao wa kampuni moja (jina tunalo) kuchota fedha za serikali unakamilika. 

``Hatua hiyo itathibitisha hisia zilizoko mitaani kuwa mtandao wa kuchota fedha za serikali unakamilika,``chanzo chetu kilimkariri mbunge huyo. 

Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, William Shelukindo, alithibitisha kumwita Ngeleja na kwamba, kilichosalia ni kusikiliza uamuzi utakaochukuliwa na serikali. 

Tayari, Kampuni ya Dowans Holding imetangaza zabuni ya kuuza mitambo hiyo, ambayo katika hitilafu iliyotokea hivi karibuni kwenye mitambo ya Songasi, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima, alisema kama hali ingeendelea kuwa mbaya walikuwa wakipanga hata kununua mitambo hiyo. 

Kashfa ya Richmond sasa Dowans, ilisababisha Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Ibrahim Msabaha na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, kulazimishwa kujiuzulu nyadhifa zao. 

Hata hivyo, miongoni mwa baadhi ya mapendekezo ambayo hayajatekelezwa ni kumuwajibisha Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Johnson Mwanyika, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi na Kamishna wa Nishati, Bashir Mrindoko. 

Jitihada za kumpata Waziri Ngeleja na Dk Rashid kutoa ufafanuzi wa suala hilo hazikufanikiwa kwani simu zao zilikuwa hazipatikani zikiashiria ama zimezimwa au ziko nje ya mtandao.

CUF kuandamana kesho

Sakata la madai ya walimu na ufungwaji wa vyuo vikuu nchini, limezidi kuzua mambo, baada ya Chama cha Wananchi (CUF), kuandaa maandamano ya amani. 

Maandamano hayo yamepangwa kufanyika keshokutwa, jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwasilisha tamko lao Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kuhusiana na kadhia hizo. 

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa CUF iliyotumwa kwa niaba yake na Kaimu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mahusiano na Umma wa chama hicho, Mbaralah Maharagande, kupitia mtandao wa kompyuta jana, maandamano hayo yanatarajiwa kuanzia katika majengo ya Karimjee saa 8:00 mchana na kwenda moja kwa moja hadi wizarani hapo. 

Taarifa hiyo inaonyesha kuwa, Waziri wa Wizara hiyo, Profesa Jumanne Maghembe, amepelekewa na chama hicho barua yenye Kumbukumbu namba CUF/AK/DSM/KR/MMU/IF/2008/43 ya Novemba 18, mwaka huu, ikimtaka apokee maandamano hayo. 

Nakala ya barua hiyo, imepelekwa pia, kwa Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Rais wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Sehemu ya Mlimani, Rais wa Wanafunzi wa Chuo Kishiriki cha Elimu Chang`ombe (DUCE) na kwa vyombo vya habari. 

CUF pia, imemwandikia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala barua rasmi, Marais wa CWT, Wanafunzi DUCE na UDSM kuwaarifu kuhusu maandamano hayo. 

Walimu wa shule za msingi na sekondari nchini, juzi walianza mgomo kushinikiza serikali iwalipe madai yao kabla ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, kuzuia kwa mara nyingine juzi mgomo huo.

Pinda Akiri Mgomo wa Walimu Umeyumbisha Nchi


WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, jana alitoboa ukweli wa athari zilizoipata serikali aliposema kuwa mgomo wa walimu umeiweka serikali mahali pabaya na kufafanua kuwa kelele zao ziliiyumbisha nchi.

Pinda ambaye ni kinara wa shughuli za serikali pia alitoa kauli iliyoashiria kuwa kiini cha mgomo wa walimu ni utendaji usio wa kuwajibika wa watendaji wa ngazi za chini wa serikali na amewaagiza wakuu wa mikoa kuhakikisha tatizo hilo halitokei tena na kuifedhehesha serikali.

Kauli ya Waziri Mkuu imekuja siku moja baada ya Katibu Mkuu Kiongozi na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Phillemon Luhanjo kutoa tamko la serikali akiwashukuru "maelfu kwa maelfu ya walimu nchi nzima" kwa kukataa "kushiriki mgomo usiokuwa na kikomo ulioitishwa na Chama cha Walimu (CWT) chini ya Mwenyekiti wake, Gratian Mukoba".

Luhanjo alitoa tamko hilo siku ambayo walimu walikuwa waanze kugoma baada ya kushinda rufaa dhidi ya amri ya kuzuia mgomo iliyotolewa na Mahakama ya Rufaa Alhamisi ya Novemba 13. Hata hivyo, mgomo huo ulianza huku kukiwa na utata baada ya Mahakama ya Kazi kutoa amri nyingine ya kuuzuia katika hukumu iliyotolewa usiku wa Novemba 17 baada ya serikali kurekebisha maombi yake ya kutaka mgomo huo uzuiwe.

Shauri hilo la serikali dhidi ya CWT litasikilizwa kesho na Mahakama ya Kazi, lakini walimu wamesema baada ya hapo, mgomo utaendelea kama ilivyopangwa.

Jana, Waziri Pinda alitofautiana kabisa na pongezi za Luhanjo akikemea na kuagiza watendaji wa halmashauri kutorudia tena uzembe uliosababisha kuwepo na malimbikizo makubwa kiasi hicho.

Waziri Pinda, ambaye katika ziara yake mkoani hapa aliulizwa juu ya mgomo huo, lakini akakataa kuuzungumzia kwa maelezo kuwa atatoa kauli baada ya mgomo kutokea, jana alionekana kuzungumza kwa uchungu sana na kukiri kuwa nchi iliwekwa mahali pagumu sana.

"Nchi itayumba kwa ajili ya kelele za walimu," alisema Waziri Pinda ambaye alikuwa akifanya majumuisho ya ziara yake mkoani Dodoma.

Pinda alionya kuwa walimu waliiweka serikali mahali pagumu sana na kuwafanya viongozi kufanya kazi kwa nguvu nyingi na kwamba kama kungekuwa na umakini, mambo hayo yasingeweza kutokea.

“Ninakuagiza (Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, William) Lukuvi, kwa niaba ya wakuu wengine wote nchini... hakikisheni kuwa watendaji wenu wa ngazi ya chini wanakuwa makini, ili kusiwe na malimbikizo ya madeni ya walimu kwa kuwa madeni yanaiweka serikali mahali pagumu sana na kwa kweli ni aibu sana.”

Pinda alisema watendaji hawana budi kuhakikisha kuwa malipo ya walimu hayalimbikizwi kiasi cha kuwa mzigo kwa taifa na kuwaagiza wakuu wa mikoa kuhakikisha wanawasimamia watendaji wa ngazi za chini ili wawe makini katika kuzuia madeni ya walimu na kuzuia tatizo kama hilo lisijirudie.

Walimu wanataka kugoma ili kuishinikiza serikali kuwalipa zaidi ya Sh16 bilioni ambazo ni malimbikizo ya malipo yao mbalimbali, lakini serikali imekuwa ikijitetea kuwa ilishalipa zaidi ya nusu ya madai hayo; kuwa madai mengi ni ya kughushi; inaendelea na zoezi la uhakiki.

Katika kuonyesha kuwa mgomo huo uliiyumbisha nchi, serikali imekuwa ikitumia kila mbinu kuhakikisha inazima jitihada za walimu kugoma na kuijeruhi serikali.

Wakati zikiwa zimesalia siku chache kabla ya siku 60 za notisi ya mgomo iliyotolewa na CWT kuisha, serikali ilikimbilia mahakamani na kufanikiwa kuuzuia mgomo huo usianze Oktoba 15 kwa amri iliyotolea na Jaji William Mandia jioni ya Oktoba 13.

Lakini CWT ikafanikiwa kutengua amri hiyo ilipokata rufaa Mahakama ya Rufaa Novemba 13 na kutangaza kuwa mgomo ungeanza tena Jumatatu ya Novemba 17. Lakini siku hiyo, shauri la serikali lilisikilizwa hadi Saa 3:49 usiku wakati Mahakama ya Kazi ilipotoa amri ya kuuzuia tena mgomo huo usiendelee Novemba 18 baada ya serikali kurekebisha maombi yake ya amri hiyo ya muda ya kusitisha mgomo.

Wakati maofisa wa serikali wakihaha mahakamani, maofisa wengine walikuwa wakihaha kuandaa malipo ya madai ya walimu hao na Jumapili ya Novemba 16, serikali ilitoa tangazo kuwa malipo yote yameshatumwa kwenye halmashauri huku ikiwasihi walimu wasianze mgomo Novemba 17 kama ilivyopangwa.

Hata hivyo, malipo hayo yanaonekana kuwa huenda yakawa chanzo cha matatizo mengine baada ya walimu kutoka mikoa kadhaa kuripotiwa kupunjwa malipo yao, huku wengine wakikuta malipo hewa.

Katika ziara yake mkoani Dodoma, mbali na kuwataka watendaji kuwa makini katika kushughulikia malipo ya walimu , Waziri Pinda amekuwa akizungumzia kwa nguvu utendaji wa watendaji hao, akiwataka wabadilike na kuwajibika kwa wananchi.

Katika hotuba yake ya majumuisho Waziri Pinda aliwataka viongozi kuwa na mikakati ya kudumu katika kuondoa kero kwa wananchi na kushirikiana na serikali katika kutatua matatizo makubwa yanayotokea hapa nchini.

Aliagiza kuwepo na mahusiano mazuri kati ya serikali kuu na serikali za mitaa, akisema kuwa zote zinafanya kazi ya kuwahudumia wananchi na ni sehemu ya serikali moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Mkuu pia alirudia kauli yake ya kuwataka Watanzania kuondoka wakijua kuwa vita kuu iliyo mbele yao ambayo wanapaswa kupigana nayo ni vita ya kilimo ambayo walisema kuwa, ni lazima kila mtu kuvaa silaha za kivita na kuingia msituni kwenda kupigana.

Aliwaagiza viongozi kutokaa ofisini na badala yake waende kwa wananchi kwa ajili ya kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi mara moja, huku akisisitiza kuwa kila mkoa ni lazima kuwe na daftari la kudumu la kilimo.

Kuhusu wakuu wa wilaya aliwaagiza kufanya mikataba na viongozi wao wa ngazi za chini, wakiwemo watendaji wa kata na vijiji, akitolea mfano wa Mkurugenzi wa Wilaya ya Chamwino ambaye amefanikiwa katika ujenzi wa shule za sekondari wilayani mwake baada ya kuwekeana mikataba na watendaji wake.

kP Leo

Mtoto wa Binadamu Alelewa na Nyani Miaka 5 Porini

WATANZANIA wameombwa kujitokeza kumsaidia kielimu mtoto Bahati Baraka Rose (11) ambaye anadaiwa kulelewa na nyani baada ya kutupwa porini akiwa mchanga wilayani Bukombe, Shinyanga.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kimanga, Tabata, Bw. Pastory Kyombya, alisema mtoto huyo kwa sasa analelewa na Bibi Rose Mbwambo wa Kimanga.

Alisema Bibi Mbwambo alikabidhiwa mtoto huyo na Serikali wilayani Bukombe baada ya kufuata taratibu zote za kiserikali.

Alisema Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukombe, Bw. Richard Nhende, ndiye aliyemkabidhi Bibi Mbwambo mtoto huyo ili amlee baada ya kumwomba.

Bw. Kyombya alisema mtoto huyo anaomba kupelekwa shule kama anavyoshuhudia wenzake wakienda shule na kuwaomba wasamaria wema wajitokeze kumsaidia ili aanze shule mwakani.

Naye Bibi Mbwambo alisema alimchukua mtoto huyo Agosti mwaka huu akiwa kwenye biashara zake Bukombe.

"Nilikuwa nimepanga kwenye nyumba ya kulala wageni ya Neema, nikiwa na wenzangu, mama mmoja (hakumtaja jina) ambaye alikuwa akitupikia chakula alitujia na kutueleza matatizo aliyonayo mtoto Baraka.

"Nilimwonea huruma sana Baraka, baada ya mama huyo kutuelezea historia yake nzima na kwamba hana ndugu na maisha yake ni ya kutangatanga na kututaka tumsaidie," alisema.

Alisema yeye binafsi aliingiwa na huruma ndipo alipofuata taratibu zote za kumchukua mtoto huyo na kuja naye Dar es Salaam kumlea.

Bibi Mbwambo alisema atamtunza mtoto huyo kama anavyotunza watoto wake ila aliomba wasamaria wema kujitokeza kumsaidia ili aanze masomo mwakani ikiwezekana shule ya bweni.

Alisema mtoto huyo alilelewa na nyani miaka kadhaa porini kabla ya kuchukuliwa tena na binadamu baada ya nyani huyo mlezi kuuawa kwa risasi.

Bibi Mbwambo alisema inadaiwa mtoto huyo aliokotwa na nyani akiwa kwenye mfuko wa 'rambo' akiwa mchanga na kumlea kwa miaka mitano.

"Askari wa wanyamapori wa Ushirombo, Bukombe, ndio waliofanikisha kupatikana kwa mtoto huyo baada ya siku moja kumwona nyani akimnyonyesha.

"Hata hivyo, inadaiwa askari hao walipata shida kumchukua mtoto huyo baada ya nyani mlezi kukimbia naye mara zote kila alipokuwa akiwaona, hivyo kuchukua muda mrefu kumpata," alisema.

Alisema mtoto huyo aliendelea kulelewa na nyani huyo hadi alipofikisha umri wa miaka mitano na baadaye askari hao kumvamia tena ili kumnyang'anya mtoto huyo na kusababisha vurugu kubwa kati yao na nyani mlezi.

Bibi Mbwambo alisema katika vurugu hizo, askari walimfyatulia risasi nyani huyo na kumuua huku risasi moja ikimpata mtoto huyo kwenye kidole cha mguu wa kushoto.

Alisema askari hao walimchukua mtoto huyo na kumpeleka katika hospitali ya Bukombe ambako aliendelea kulelewa hospitalini hapo.

Bibi Mbwambo alisema watu mbalimbali walikuwa wakimchukua mtoto huyo na kumlea na walioshindwa walikuwa wakimrudisha hospitalini hapo, lakini msamaria mwema alimchukua, lakini mtoto huyo alimtoroka na kuingia mitaani na kuishi maisha ya shida.

Alisema Baraka alikwishazoea kuishi maisha ya porini, akiparamia miti na kusababisha wasamaria wema waliokuwa wakimlea kulazimika kumfunga minyororo ili asitoroke.

Juma Nature Ageuka Kivutio Kizimbani

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Temeke jana, ilisheheni umati wa watu, wakiwemo wazazi wa Msanii wa Muziki wa Kizazi kipya ( Bongo fleva) jijini Dar es Salaam, Juma Kassim Nature, (28) akikabiliwa na tuhuma za kumbaka Mwanafunzi wa Kidato cha tatu (16) kwa zamu.

Tuhuma hiyo, inamuhusisha pia Godwine Malima (26), ambaye ni Mwalimu anayekabiliwa na tuhuma za kumbaka mwanafunzi huyo na kumchukua kwenda kuishi naye kinyume na ridhaa ya wazazi.

Hata hivyo Nature, alifikishwa mahakamani hapo, akiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke Emmanuel Kandihabi, majira ya saa 4:15, alipokuwa akishikiliwa na hatiani katika kituo cha Changombe cha Wilaya hiyo.

Aidha mara tu baada ya kumfikisha mahakamani hapo, Kandihabi, alisisitiza kuwa ni lazima msanii huyo, asomewa mashtaka yake leo, ili hatua za kisheria zichuke mkondo wake.

Mara baada ya msanii huyo kufikishwa mahakamani hapo, na mwenzie kwa ajili ya kusomewa mashtaka yanayo wakabili, mahakama ilionekana kujaa na umati mkubwa uliokusanya watu mbalimbali wakiwemo wasanii wake pamoja na familia yake.

Hata hivyo, msanii huyo alipandishwa kizimbani majira ya saa 8:15 kwa ajili ya kusomewa shataka la kubaka linalomkabili, akiwa amaeambatana na mshtakiwa mwenzie ambae anakabili na tuhuma za kumchukua mwanafunzi huyo na kwenda kukaa naye kinyume na ridhaa ya wazazi wake.

Aidha Mwendesha Mshtaka, Mrakibu wa Polisi Basill Pandisha, alisema kuwa washtakiwa hao, walitenda kosa hilo mnamo Novemba 1 mwaka huu eneo la Sugar Rays, jijini Dar es Salaam, na kudai kuwa, mtuhumiwa namba moja ambaye ni Juma Kassim alimbaka mwanafunzi huyo bila ya ridhaa yake, huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Ilidaiwa katika maelezo ya malalamikaji kuwa, mnamo majira ya saa 1:40 usiku maeneo ya Sugar Rays, mlalamikaji alikuwa ameenda kwa mtuhumiwa kwa lengo la kuzungumza naye, kwani wiki mbili zilizopita mtuhumiwa alikuwa akimsumbua kupitia namba yake ya simu.

Ilielezwa kuwa, mlalamikaji alipofika nyumbani kwake alimkuta rafiki yake Godwine Malima ambaye ni mshtakiwa wa pili na kudai mtuhumiwa hayupo hivyo aliamua kumsubiri.

Hata hivyo ilielezwa kuwa, wakati mlalamikaji akiendelea kumsubiri ghafla mtuhummiwa namba mbili, alimwambia mwanafunzi huyo, waende naye na walifikia katika vyumba vya kulala wa geni, iliyoko Sugar Rays, ndipo alipofika Juma Kassim na kuzungumza naye.

Katika kosa la pili Pandisha aliieleza mahakama kuwa mnamo mmuda na majjira yanayofanana, mshtakiwa namba mbilii, Godwine Malima, anatuhumiwa kintume nasheria kumchukua mlalamikaji huyo, na kwenda naye nyumbani kwake, bila ya ridhaa ya wazazi wake, huku akijuafika kuwa ni mwanafunzi na anaumri wa miaka chini ya 18.

Watuhumiwa kwa pamoja walikana shtaka hilo, na kupewa dhamana kwa mmasharti ya kuleta mdhamini mmoja mwenye mali isiyo hamishika, na mfanyakazi wa serikali kwa dhamana ya shs. 5 milioni.

Hata hivyo, mtuhumiwa namba moja, Juma Kassim alipewa dhamana baada ya kuweza kutimiza masharti ya dhamana, huku mwenzie akionekana kusuasua baada ya wadhamini wake kutokuleta barua ya dhamana.

Hakimu Riwa, alimwambia mtuhumiwa namba mbili,, mahakam iko tayari kumsubiri wadhamini wafuatilie kitambulisho pamoja na barua ya udhammni inayoonyesha kweli maeajjiliwa na Serikali, n aakichelewa atlazimika kwenda mahabusu.

Baada ya kusomewa mashtaka watuhumiwa hao, na kupewa dhamana, kwa Juma Nature, Mwanachi ijaribu kuzungumza na Wazazi wake lakini walionekana kujawa na simmanzi kubwa na hawakuwa tayari kuzungumza lolote.

Aidha , Mwananchi haikukata tamaa, baada ya wazazi hao, kukataa kabisa kuzungumza na waandishi,bbali irusha tena kombola kwa wasanii wenzie waliokuwa wafika mahakamni hapo kwa ajili ya kuju hatma ya Kamanda wao katika fani ya muziki, na pia walionyesha kukataa kabisa kuzungumza.

Hata hivyo alisikika msanii mmoja miongoni mwao, alimkazia macho Mwandishi wa hababri hizi, na alipoulizwa swali alisikika akijibu kuwa unataka kujua jina langu ili iweje , na kuonyesha kukerwa na swali lile na kuendelea kuongea kwa ukali huku akimuuliza, unanijua mie ni nani, sina muda wa kuzungummza nawe alidai msanii huyo.

Wafungwa wapigwa vibaya mno Kenya


Msemaji wa idara ya magereza nchini Kenya, amesema ameshangazwa na video ambayo inaonyesha maafisa wa magereza wakiwapiga kikatili wafungwa gerezani, na uchunguzi umeanzishwa mara moja kuhusiana na tukio hilo.

Mfungwa mmoja alifariki kutokana na ukatili huo, na wafungwa wenzake wanasema kifo hicho kilitokana na kipigo alichofanyiwa na maafisa wa magereza.

 Yeyote anayezingatia haki za kibinadamu atashtushwa na yaliyotokea
 
Dickson Mwakazi msemaji wa Idara ya Magereza nchini Kenya

Picha hiyo ya video iliyonaswa kwa kutumia simu ya mkononi, inaonyesha wafungwa walio uchi katika jela yenye ulinzi mkali ya Kamiti, wakitandikwa kwa rungu na mijeledi.

Haijafahamika kama picha hizo zilipigwa na mfungwa au afisa wa magereza aliyekuwa na huruma.

Wafungwa hao walipigwa wakati maafisa wa magereza walikuwa wakiendesha oparesheni ya kuwapokonya simu wafungwa.

Wafungwa nchini Kenya hawaruhusiwi kumiliki au kutumia simu.

Meli ya Maharamia Yazamishwa Aden

Manuwari ya India imeangamiza meli moja ambayo inashukiwa ilikuwa na maharamia wa Kisomali, katika ghuba la Aden.

Manuwari hiyo, INS Tabar, ilibidi kuizamisha meli hiyo iliyokuwa na watu wanaoshukiwa kuwa ni maharamia, baada ya kukataa kuisimama ili meli kuchunguzwa, na badala yake walianza kufyatua risasi.

Habari hizi ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wanamaji wa India.

Kumekuwa na visa kadha vya meli kutekwa na maharamia hivi majuzi, katika pwani ya Somalia.

Kisa kilichotokea hivi karibuni kilifanyika siku chache baada ya meli ya Saudi Arabia, Sirius Star, yenye shehena ya mafuta ambayo hayajasafishwa, na wafanyakazi 25, kutekwa na maharamia na kuelekezwa kutua nanga katika pwani ya Somalia.

Sirius Star

Vela International, kampuni ambayo inasimamia safari za meli hiyo ya Sirius Star, imeielezea BBC kwamba kufikia sasa hakuna matakwa yoyote ya fidia yaliyotolewa na maharamia hao.

Kampuni hiyo pia ilielezea kwamba wafanyakazi wa meli hiyo wote wako salama.

Meli hiyo imebeba mapipa milioni mbili ya mafuta ambayo hayajasafishwa, na yenye thamani ya dola milioni 100 za Kimarekani.

Friday, November 14, 2008

Majeshi ya kigeni yaonekana Congo.

Ushahidi umeongezeka kwamba kuna majeshi ya kigeni yaliyoingia katika mgogoro wa kivita mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Watu walioshuhudia wameiambia BBC, wamewaona wanajeshi wa Angola na Zimbabwe.

Wakati huo huo waandishi wa habari wametangaza baadhi ya askari wa Jenerali muasi Laurent Nkunda bado wanalipwa mishahara yao na jeshi la Rwanda.

Hii imezusha tena hofu mapigano hayo huenda yakawa kama marudio ya vita vya miaka mitano nchini humo, ambavyo vilihusisha nchi 8 kabla ya kumalizika mwaka 2003.

Watu wapatao 250,000 walikimbia mapigano makali ya hivi karibuni yaliyoanza kupamba moto mwezi Agosti, baina ya majeshi ya Serikali na waasi wanaodai kujilinda dhidi ya waasi wa kihutu kutoka Rwanda waliokimbilia nchini Congo baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Wanajeshi hao wanafanya doria lakini hawawezi kuwasiliana na wananchi kwa sababu wanazungumza Kireno.

Friday, November 7, 2008

Pinda Akabidhiwa 'Kitanzi' Cha Makamba

SHINIKIZO la wabunge wa CCM la kutaka kung’olewa kwa Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusuph Makamba, limechukua sura mpya baada ya wabunge wa chama hicho kuwasilisha hoja hiyo kwa Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM, Bw. Mizengo Pinda, kwa madai kuwa anakigawa chama. 

Hatua hiyo ilijitokeza juzi jioni katika kikao cha wabunge hao ambacho kilipangwa kufanyika saa 10 jioni, lakini kikachelewa kutokana na mgongano wa wabunge hao ambao baadhi ya hoja zilizokuwa mezani lizipingwa. 

Kwa mujibu wa chanzo cha habari cha kuaminika kutoka ndani ya chama hicho, katika mambo yaliyozungumzwa ni hoja ya kutaka kung’olewa kwa Bw. Makamba katika kiti hicho, kwani amekuwa akifanya mambo yanayowagawa wana CCM. 

“Hoja hii tumeifikisha kwa Mwenyekiti wetu ambaye naye anasema hawezi kutoa jibu, bali atalifikisha kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, ambaye ni Rais Jakaya Kikwete,” kilisema chanzo hicho. 

Sababu za kutaka aachie nafasi hiyo ni madai ya kupokea wanachama kutoka vyama vya upinzani na kuwapa madaraka makubwa bila uchunguzi wa kutosha. 

“Mbali na hili, jingine ni la Tarime ambako alipeleka watu wasiokuwa na uzoefu wa kutosha katika masuala ya kampeni, lakini kubwa zaidi alifikia kwa mwanachama mmoja kitendo kilichowakera wana CCM wengine na kwa kufanya hivyo, ni kuwagawa wanachama,” kilisema chanzo cha habari. 

Tuhuma nyingine ya Bw. Makamba ni kuwachonganisha wabunge hao na wananchi kwa kile alichokitangaza kuwa hawaendi majimboni mwao. 

Suala lingine lililoibuka ndani ya mkutano huo, ni wabunge hao kupendekeza baadhi ya mawaziri wenye nyadhifa kubwa ndani ya chama, kuchagua suala moja la ama kuachia ngazi ya uwaziri au nafasi ya uongozi katika chama. 

“Wapo hawa mawaziri hawana muda sasa wa kukitumikia chama vizuri, hivyo ifike mahali wachague kitu kimoja, kwani lengo letu sasa ni kukijenga chama na si kuendelea kukibomoa,” kilisema chanzo kingine cha habari. 

Kitu kingine kilichoibuka ni wabunge wa viti maalumu kuingilia wenzao katika majimbo yao, hali inayoleta picha mbaya na kuonesha tamaa ya madaraka. 

Masuala haya mazito yalijitokeza wakati wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wanatarajia kuanza mkutano wao mjini hapa kesho, ambao unatarajiwa kuwa na ajenda nzito. 

Akizungumza juzi na gazetihili, Bw. Makamba alikanusha kuwapo kwa mpango huo, akisema ni hisia za mtu mmoja na kama zingekuwa za wabunge wa CCM angeshapata taarifa. 

Alitaka mawazo hayo yachukuliwe kama masuala ya mitaani na kwamba vikao maalumu ndivyo vinavyoweza kuamua hatima yake. 

Baadhi ya viongozi waliotoka Upinzani na kupewa nyadhifa ndani ya CCM ni Bw. Tambwe Hiza aliyekuwa CUF, Bw. Salum Msabah kutoka CUF na wengineo.

Obama Atazamiwa Kutangaza Baraza Lake

Barack Obama ameanza kuunda serikali yake kwa kumuomba aliyekua mshauri wa Rais Clinton Rahm Emanuel, kuwa mnadhimu wa Ikulu ya Marekani.

Rais mteule Obama anatazamiwa kumteua Waziri wa fedha ambaye jukumu lake kuu ni kukabiliana na hali mbovu ya uchumi.

Licha ya kuanza mapema bado Bw.Obama ana mda hadi tarehe 20 januari mwakani kuchagua baraza lake la mawaziri.

Bw.Obama alichaguliwa kua raia wa kwanza mweusi kuliongoza taifa kubwa duniani akimshinda mpinzani wake kutoka chama cha Republican l John McCain.

Uongozi wa mpito wa Bw.Obama utaongozwa na John Podesta, aliyekuwa mnadhimu wa Ikulu chini ya utawala wa Rais Clinton, pamoja na Pete Rouse, ambaye alikua mnadhimu mkuu wa Seneta wa Bw.Obama.

Hakuna tangazo lolote linalotarajiwa leo alhamisi kuhusiana na shughuli za Bw.Obama lakini wafanyikazi wa Bw.Obama wamesema anatarajiwa kuhutubia wandishi wa habari kabla ya mwisho wa juma hili.

Miongoni mwa nyadhifa kubwa zinazohitajika ni Waziri wa mashauri ya kigeni, Ulinzi na hazina.

Bw.Obama amedokezea kwamba anaweza kumuachia wadhifa wa Wizara ya Ulinzi waziri wa sasa Robert Gates katika moyo ule wa utangamano kama alivyoahidi kuchagua kutoka vyama vyote. Kamanda huyu anasifika kwa mpango wake wa kuongezea idadi ya vikosi nchini Iraq, hatua iliyopunguza ghasia huko.
Mojapo ya ahadi za Barack Obama katika sera yake ya kigeni ni kuyaondosha majeshi ya Marekani huko Iraq katika kipindi cha miezi 18.

Wafanyabiashara Waanza Kushusha Bei ya Mafuta

Mamlaka wa Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), imesema baadhi ya wafanyabiashara wa bidhaa za petroli wameteremsha bei licha ya kuwa wako baadhi ambao hawajafanya hivyo kwa visingizio kadhaa. 

Mkurugenzi wa Ewura, Haruna Masebu alisema jana kuwa wafanyabiashara ambao hawajapunguza bei hizo ni wale ambao bado wanabishana na Ewura juu ya fomula inayotumika kuuzia mafuta na wengine wanatoa visingizio vya kuwa na akiba ya mafuta waliyoagiza siku za nyuma kabla ya bei kushuka. 

Alisema baada ya barua ile iliyoandikwa na Ewura kwenda kwa wafanyabiashara, wengine walionyesha wasiwasi wa kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya dola ya Marekani ambayo kwa dola moja ni Sh 1,300. “Lakini wengi wameshusha bei na ninyi ni mashuhuda… katika baadhi ya vituo, bei zimeshuka hadi shilingi 1,500 kwa petroli, dizeli inauzwa shilingi 1,575 na mafuta ya taa 1,290,” alisema Masebu. 

Alivitaja baadhi ya vituo kama vya BigBon, Total, Mt. Meru na Gapco kuwa vimeteremsha bei. Lakini hata hivyo, alikiri kuwa vituo kama vya BP havijateremsha bei kwa kisingizio cha kuwa na akiba ya mafuta ya nyuma. 

Alisema licha ya bei ya mafuta kushuka katika soko la dunia, lakini bei za usafirishaji, bima (CIF) na gharama za bandari, ziko palepale hali inayowalazimu wenye vituo vya mafuta kuendelea kuuza kwa bei kulingana na gharama hizo. 

Alisema wakati wamewaandikia barua wafanyabiashara, baadhi waliahidi kuteremsha, lakini wakaomba kufanyike fomula mpya ya kupata vigezo vya bei ya mafuta, wengine wakasingizia kushuka kwa thamani ya shilingi pamoja na kodi mbalimbali zinazotozwa nchini. 

Alisema Ewura inatambua kuwapo kwa mafuta yaliyoagizwa siku za nyuma, lakini akaonya kuwa Ewura haitasita kuchukua hatua iwapo wafanyabiashara hao wataendelea kudanganya kwa kisingizio hicho. “Mamlaka yetu inafuata sheria katika kutekeleza udhibiti, hakuna mfanyabiashara aliye juu ya sheria, wale ambao wataendelea kukaidi kushusha tutaangalia sheria inavyosema,” alisema Mkurugenzi huyo.

Wakimbizi Watimuliwa na Waasi Congo.

Mashambulio ya waasi mashariki mwa DR Kongo yamewalazimisha maelfu ya raia wa mji uliokuwa mikononi mwa wanamgambo wanaiunga mkono serikali kuukimbia.

Waasi waliuteka mji wa Kiwanja baada ya siku ya pili ya mapigano na wapiganaji wa kundi liitwalo Pareco Mai-Mai. Baada ya mapigano hayo waasi waliwaamuru raia wa mji huo kuondoka ili wafanye kazi ya upekuzi.

Kiongozi wa waasi Jenerali Laurent Nkunda ameishutumu serikali kwa kuvunja makubaliano ya kusimamisha mapigano yaliyotangazwa wiki iliyopita.

Takriban watu 250,000 wamezikimbia nyumba zao kutokana na mapigano hayo.

Wanawake na watoto ni wengi zaidi walioamriwa kuuhama mji wa Kiwanja siku ya Jumatano.

Thursday, November 6, 2008

Goma, MONUC Yajikuta Katika Mapigano

Umoja wa Mataifa umesema askari wake wamejikuta katikati ya mapigano baada ya vita kuzuka mashariki mwa DR Congo baada ya siku chache za kusitishwa mapigano.

Msemaji wa umoja wa mataifa mjini Goma amesema kumekuwepo na mapigano baina ya majeshi ya waasi na makundi mawili ya wanamgambo ambayo yanaunga mkono serikali.

Wiki iliyopita, kiongozi wa waasi Jenerali Laurent Nkunda alitangaza kusitisha mapigano wakati vikosi vyake vilipoukaribia mji wa Goma.

Mwandishi wa BBC mjini Goma, Peter Greste amesema bado kuna tishio la kuzuka upya mapigano.

Mji wa Goma umezingirwa na majeshi ya waasi ambayo yaliyafukuza majeshi ya serikali.

Watu wapatao 250,000 waliyahama makazi yao na mashirika ya misaada yanaendelea kujitahidi kuwasaidia.

Baadhi walikimbia vijiji vyao na kuelekea mjini Goma, lakini wengine wamesharudia baada ya kukosa chakula cha kutosha na mahema huko mjini.

Hapo awali, waziri wa mashauri ya kigeni wa Ufaransa alitoa wito wa kuimarisha kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa chenye askari 17,000 hivi sasa.

Hotuba Ya Obama Mara Baada ya Matokeo ya Uchaguzi Wa Rais

Watuhumiwa wa EPA watinga mahakamani

HATIMAYE mafisadi wanaotuhumiwa kuchota mabilioni ya fedha kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), jana walifikishwa mahakamani na kufunguliwa mashitaka ya kughushi na kujipatia mamilioni ya fedha toka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Jumla ya watu 10, akiwemo mfanyabiashara maarufu Jayantkumar Chandubhai Patel, maarufu kwa jina la Jeetu Patel, pamoja na wafanyakazi wa BoT walifikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kesi hiyo ya aina yake ilishuhudiwa na wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake ilichukua zaidi ya saa tano na kumalizika saa 11:45 jioni wakati muda wa kazi unaisha saa 10.30 jioni.

Washitakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa nyakati tofauti huku mshitakiwa namba moja katika kesi hiyo, Johnson Lukaza akipandishwa peke yake kujibu tuhuma za kula njama na kughushi na kuiibia BoT zaidi ya Sh6.3 bilioni.

Mbele ya Hakimu, Euphemia Mingi, wakili wa serikali Winie Koroso alidai kuwa, kati ya Desemba 2003 na 2005 mshitakiwa alighushi hati ya kuhamishia mali toka kampuni ya Kernel na Maruben ya nchini Japan ambayo ilikuwa inaonyesha imetolewa Februari 4 mwaka 2005.

Koroso alidai kuwa baada ya kughushi hati hiyo aliiwasilisha BoT jijini Dar es Salaam na kujipatia kiasi hicho cha fedha.

Hata hivyo, mshitakiwa huyo alikana shtaka hilo na Hakimu Mingi aliahirisha kesi hiyo mpaka Novemba 18 itakapotoa maamuzi ya dhamana.

Katika kesi nyingine washitakiwa watatu akiwemo Jeetu Patel na ndugu zake wawili Devendra Patel na Amit Nandy walipandishwa kizimbani kujibu tuhuma za kula njama na kuiibia BoT zaidi ya Sh 2.5 bilioni.

Washitakiwa hao, ambao walifikishwa mbele ya Hakimu Neema Chusi, kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Agosti 7 na Desemba 7 mwaka 2005 jijini Dar es Salaam walikula njama za kuiibia BoT Sh2,599,944,456.12 na kuziwakilisha katika kampuni ya Matsushita Electric Trading.

Katika kesi hiyo mshitakiwa wa tatu Amit Nandi anadaiwa kughushi hati iliyoonyesha kuwa kampuni hiyo ya Matsushita inaidai BoT kiasi hicho cha fedha.

Wakili Koroso aliendelea kudai kuwa Septemba 2 mwaka 2005 washitakiwa walikula njama ya kuiibia BoT Sh3.9 bilioni baada ya kusaini mkataba kati ya kampuni ya Bina na C. Itoh za nchini Japan.

Washitakiwa hao walikana mashtaka yao na mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi leo itakapotoa maamuzi ya dhamana.

Mfanyabiashara huyo mwenye asili ya Kiasia pia alipandishwa kizambani tena na ndugu zake watatu, wakiwemo wawili wa awali na Ketan Chohan aliyeongezeka wakikabiliwa na tuhuma za kughushi mkataba wa Kampuni ya Bina Resort na Itoh wakituhumiwa kula njama na kuibia BoT zaidi ya Sh3.9 bilioni.

Pia wafanyakazi watano wa BoT, akiwemo mtu na mke wake, walipandishwa kizimbani kujibu tuhuma za kula njama ya kuiibia benki hiyo.

Washitakiwa hao ni pamoja na Bahati Mahenge, Manase Mwakale, Devis Kamungu, Godfrey Moshi na Iddah Mwakale, ambao kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Desemba 23 mwaka 2003 na Oktoba 26 2005 jijini Dar es Salaam walikula njama za kuiibia BoT.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kugushi mkataba wa makubaliano wa kampuni ya Changanyikeni kwa kutumia saini ya meneja wa kampuni hiyo, Samson Mapunda na kujipatia Sh 8.5 bilioni mali ya BoT, lakini walikana mashitaka yao na kurudishwa tena rumande hadi leo mahakama itakapotoa maamuzi ya dhamana.

Hata hivyo ni makampuni machache kati ya makapuni yaliyohusika katika wizi huo ambayo jana yalitajwa kuhusika na wizi huo.

Kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa hao kunatokana na ya mafisadi hao walioshindwa kurejesha sh 64 bilioni kati ya sh 133 bilioni zilizochotwa kwenye akaunti hiyo.

Macho ya wengi yalikuwa kwa mtuhumiwa Jeetu Patel, ambaye alionekana kuwa kigogo pekee kati ya wafanyabiashara kumi waliofikishwa mahakamani jana.

Kilichovutia zaidi ni namna Jeetu alivyokamatwa. Kukamatwa kwake kunaonekana kulipangwa kisayansi kwa kutumia mbinu mahiri za kikachero ambazo zilipangwa na Kurugenzi ya Upelelezi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ya Jeshi iliyo chini ya Robert Manumba na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma (DPP).

Taarifa ambazo zilipatikana jijini Dar e s Salaam jana zinasema kukamatwa kwa Jeetu kulifanywa kwa siri kubwa, kiasi cha mfanyabiashara huyo kutohisi lolote.

Duru hizo za kiserikali zililidokeza gazeti hili kwamba, jana, mnamo saa 4:00, asubuhi Jeetu alipigiwa simu akaelezwa kwamba anahitajika kwa DPP, Eliazer Feleshi ambaye alikuwa pamoja na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba.

Wakati Jeetu akiwa anasita, alipigiwa tena simu akisisitiziwa kuhitajika kwa DPP na DCI ambao walikuwa wakimsubiri kwa ajili ya mazungumzo.

"Alipigiwa simu asubuhi, akaelezwa kuwa anapaswa kuja kwa DPP na DCI wako wanamsubiri. Mara ya kwanza akawa ana sitasita kuja; akapigiwa tena kuelezwa kwamba DCI na DPP walikuwa wakimsubiri hivyo anapaswa kwenda," zilisema duru hizo za kiserikali na kuongeza:

"Hakuwa akijua kabisa kwamba atapandishwa mahakamani. Alivyofika tu akaelezwa anapaswa kwenda mahakamani kusomewa mashitaka, hivyo ndivyo jinsi alivyokamatwa Jeetu."

Jeetu na makampuni yake tisa anatuhumiwa kujipatia Sh10.3 bilioni kwa madai ya kutumia nyaraka na kumbukumbu za kughushi, kitu ambacho ni kosa la jinai.

Duru nyingine zilisema mbali ya Jeetu, hata mtuhumiwa Johnson Rwekaza hakuwa akijua bali alipigiwa simu asubuhi na kuelezwa anapaswa kupanda kizimbani.

Duru hizo ziliongeza kwamba, watu wengine watano wa kampuni ya Changanyikeni Residential Complex, walijisalimisha wenyewe polisi kwa ajili ya kufikishwa mahakamani.

"Hawa wa Changanyikeni Complex walijisalimisha wenyewe baada ya kupata taarifa kwamba, wanahitajika kwa ajili ya kufika mahakamani kusomewa mashitaka," ziliongeza duru hizo.

Watuhumiwa hao na wengine kumi jana walipelekwa rumande na msafara wa magari manne ambao uliondoka Mahakama ya Kisutu mnamo saa 12:30 jioni huku ukiwa na askari wenye silaha katika magari mawili aina ya Land Rover, Defender.

Msafara huo uliongozwa na makechero waandamizi ambao walikuwa wametanda katika Mahakama ya Kisutu saa mbili kabla ya watuhumiwa kufikishwa mnamo saa 7:00 mchana.

Kufikishwa mahakamani kwa akina Jeetu ni ahadi ya Rais Jakaya Kikwete, ambaye alionya kwamba, wafanyabiashara ambao wangeshindwa kurejesha fedha ifikapo Oktoba 31, walipaswa kufikishwa kizimbani ifikapo Novemba mosi.

Tuesday, November 4, 2008

Walinzi Wauawa Wakiwa Lindoni

Walinzi wawili wameuawa katika wilaya za Pangani mkoani Tanga na Musoma Mkoa wa Mara, katika matukio ya mauaji yaliyotokea mwishoni mwa wiki wakiwa lindoni. Wilayani Pangani, mtu aliyetambuliwa kuwa ni Enock Kisali (33), mlinzi katika shamba la mkonge la Mwera Estate lililopo Kijiji cha Tungamaa wilayani humo, ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali ubavuni na watu wasiojulikana. 

Akithibitisha mauaji hayo ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Simon Sirro, alisema tukio hilo lilitokea Novemba mosi, mwaka huu majira ya usiku wakati marehemu akiwa lindoni kwake. Alisema Novemba 2, mwaka huu, majira ya saa 5.00 za asubuhi Polisi wilayani humo walipata taarifa kutoka kwa raia wema waliouona mwili wa Kisali ukiwa umetelekezwa kichakani karibu na shamba hilo. 

Alisema baada ya Polisi kupekua mwili huo, walibaini kwamba marehemu alichomwa na kitu hicho chenye ncha kali na pia alikuwa amenyongwa shingo. Alisema chanzo cha kifo hicho hakijafahamika. Wilayani Musoma, watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamemuua kwa kumchinja mlinzi wa Kimasai aliyekuwa akilinda duka la mfanyabiashara Crismas Manyama. 

Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Mara, Deus Kato alisema tukio hilo limetokea juzi usiku katika eneo la Bweri nje kidogo ya Mji wa Musoma, likimhusisha Emmanuel Rembu (30). Kato alisema mlinzi huyo alichinjwa na kwamba baada ya mauaji hayo, majambazi hao waliumwagia ukuta wa duka hilo maji ambayo yaliwarahisishia kazi ya kubomoa matofali kisha kuingia ndani na kupora vitu mbalimbali ambavyo thamani yake haijajulikana. Kaimu Kamanda huyo ambaye pia ni Ofisa Upelelezi wa Mkoa wa Mara alisema maiti ya mlinzi huyo ilitelekezwa na kukutwa asubuhi yake na watu waliokuwa wakipita maeneo hayo wakienda katika shughuli zao za kila siku. Hakuna aliyekamatwa hadi sasa.

Msinione Kimya ni Utawala Bora - JK

RAIS Jakaya Kikwete amesema uvumilivu na uhuru unaoonyeshwa na serikali yake katika nyanja mbalimbali nchini, ni mkakati wa kujenga jamii yenye utawala bora.

“Baadhi ya watu wanaiona hali hiyo kama ukosefu wa nidhamu, lakini huu ni mwelekeo wetu wa makusudi ili kujenga uvumilivu na uhuru mpana zaidi na bila shaka tutafika,” Rais Kikwete alimweleza Malkia ll Henrik wa Denmark, jana Ikulu jijini Dar es salaam.

Rais alikuwa anazungumza na malkia huyo aliyko nchini kwa ziara ya kiserikali ya siku nne baada ya kualikwa na Rais Kikwete.

Ziara hiyo ilianza jana baada ya malkia huyo kupokelewa katika sherehe ya kuvutia kwenye viwanja vya ukumbi wa Karimjee jijini.

Rais alimwambia malkia huyo kuwa hatua ya serikali za kujenga uvulivu zinachukuliwa kwa makusudi pamoja na kufahamu kwamba demokrasia nchini Tanzania bado ni changa.

“Tunajua kuwa demokrasia yetu ni changa kabisa, ndio kwanza tumeanza safari ndefu ya kujenga mfumo huo, lakini tunachukua hatua hiyo kw amanufaa ya taifa,” Rais Kikwete alimweleza mgeni wake na kuongeza:

“Tunaishukuru sana Denmark kwa kutuunga mkono katika eneo hilo, kama mnavyofanya katika maeneo mengine hasa ya maendeleo kama miundombinu, jitihada za kupambana na umasikini, virusi vya ukimwi, kufutiwa madeni na utawala bora,” alisema Rais Kikwete.

Rais pia alimshukuru Malkia kwa msaada wa Denmark kwa benki ya CRDB.

“Tunaishukuru Serikali ya Denmark na wananchi wake kwa kusaidia kuunga mkono benki ya CRDB ambayo sasa imekuwa moja ya benki bora zaidi nchini kutokana na msaada wenu,” alisema.

Rais Kikwete alimwweleza Malkia huyo kwamba kwa kiasi fulani, ziara hiyo imemkamilishia historia.

''Januari 10, mwaka 1970, nilimpokea baba yako, Mfalme Frederick wa Tisa wakati alipokuja kufungua Kituo cha Elimu cha Kibaha, kilichogharimiwa na nchi za Nordic.''

''Wakati huo nilikuwa mwanafunzi pale Kibaha Sekondari na nilijipanga mstari wa mbele kumshangilia Mfalme alipowasili. Ni jambo la ukumbusho kwamba leo nakupokea wewe mtoto wa Mfalme Frederick, ukiwa tayari Malkia. Kwa hakika mzunguko wa historia umekamilika.''

Rais Kikwete pia ameishukuru Serikali ya Denmark kwa kumteua (yeye) kuwamo katika Tume ya Ajira kwa Afrika iliyoteuliwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo.

Monday, November 3, 2008

Chama Kipya Chaipa Changamato ANC

Kundi lililojitenga kutoka chama tawala cha Afrika Kusini, African National Congress, ANC linatarajiwa kujiandikisha kama chama.

Chama cha South African Democratic Congress, SADC kinaundwa na waliokuwa wanachama wa ANC waliokihama chama hicho baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Thabo Mbeki kujiuzulu mwezi Septemba.

Katika mkutano wa kitaifa uliofanyika mwishoni mwa juma chama hicho kipya kimekishutumu chama cha ANC kwa kudhoofisha demokrasia nchini humo.

Kiongozi wa ANC, Jacob Zuma amesema anaamini chama chake kitashinda katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.

Chama cha SADC kinaongozwa na Mosiuoa Lekota, aliyekuwa waziri wa ulinzi wa nchi hiyo na mwenyekiti wa ANC.

Naibu wake atakuwa Mbhazima Shilowa, ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu wa jimbo la Gauteng.

SADC inatarajiwa kujiandikisha rasmi kama chama katika tume huru ya uchaguzi nchini humo siku ya Jumatatu.

Lipumba: Kikwete Ameonesha Woga


CHAMA cha Wananchi CUF kimesema kuwa kitendo cha Rais Jakaya Kikwete ‘kuyumba’ katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi Oktoba kuelezea kwa ufasaha suala la Tanzania kujinga na Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC) kitaleta mtafaruku nchini. 

Mwenyekiti wa Chama hicho Profesa Ibrahim Lipumba alisema hayo juzi wakati akihutubia maelfu ya wafuasi wa chama hicho kwenye uwanja wa Tropikana,Mabawa jijini Tanga 

Alisema kuwa Tanzania kujiunga na OIC sio jambo la kushangaza kwani taytari nchi 22 zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara zimeshajiunga na umoja huo kutokana na marais wa chi hizo kuridhia. 

Alizitaja baadhi ya nchi hizo zilizojiunga na OIC kuwa ni pamoja na Uganda, Msumbiji, Mali, Togo, Gabon, Senegal, Nigeria, Benini, Burkinafaso na Mauritania. 

“Kwa mfano Uganda na Msumbiji ni miongoni mwa nchi zenye wakristo wengi na hata marais wao ni wakristo lakini wameridhia kujiunga na OIC, kwa nini sisi tusijunge? alihoji, Prof. Lipumba. 

Alisema kuwa katika hotuba yake Rais Kikwete alipaswa awafafanulie vizuri maaskofu waliopinga OIC kwamba haina madhara yoyote na kwamba kuinga huko hakumaanishi kwamba ‘utasilimishwa’ bali ni kuwepo maendeleo ya kiuchumi. 

Aliongeza kuwa Visiwa vya Zanzibar asilimia kubwa ya wananchi wake walisharidhia kujiunga na OIC tangu mwaka 1993 chini ya Rais wa wakati huo, Dkt. Salmin Amour. 

“Rais mwoga katika uamuzi ni hatari sana kwani anaweza kujeta mgawanyiko ndani ya jamii kwa kushindwa kutoa uamuzi katika jambo lililodhahiri,” aliongeza. 

Katika hotuba yake Rais aliwaasa wananchi watulie wakati huu ambapo bado Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje inafanya utafiti kuona faida na hasara za kujiunga na OIC. 

Awali wiki iliyopita, Membe aligusia wakati akizungumza na waandishi wa habari kuwa utafiti umeonesha kuwa OIC ni jumuiya nzuri na kuonya watanzania waache kuwa na woga. Hata hivyo kauli hiyo ilionekana kuwakera maaskofu ambao walimpinga na kumshinikiza ajiuzulu ili "apate mufa wa kushabikia zaidi masuala ya kidini."

Wizi wa EPA: Nitachambua Faili Moja Baada ya Jingine Asema DPP

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) amesema atachambua kwa makini "faili moja baada ya jingine" baada ya kukabidhiwa rasmi mafaili ya wezi wa fedha kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na hivyo kufanya uwezekano wa watuhumiwa hao kufikishwa mahakamani katika siku chache zijazo kuwa mdogo.

Kuwasilishwa kwa mafaili ya mafisadi hao walioshindwa kurejesha Sh64 bilioni kati ya Sh133 bilioni zilizochotwa kwenye akaunti hiyo, kunafanya mzigo huo sasa uelemee kwa DPP, Eliezer Felesh ambaye ofisi yake ilikabidhiwa mafaili hayo jana na Mwanasheia Mkuu wa Serikali.

Hatua hiyo imekuja wakati hali ikiwa tete kutokana na wananchi wa kada mbalimbali, wakiwemo wabunge na wasomi kutaka wezi wote wa fedha hizo wafikishwe mahakamani tofauti na agizo la Rais Jakaya Kikwete kuwa wale ambao wangeshindwa kurejesha fedha hizo kabla ya Oktoba 31 tu ndio wafikishwe mahakamani.

Kwa mujibu wa duru mbalimbali za kiserikali, kazi kubwa iliyopo sasa inafanywa na Kurugenzi ya Upelelezi ya Makosa ya Jinai ambayo imeelezwa kuwa tayari imewaweka chini ya ulinzi watuhumiwa ikisubiri kuwafikisha mahakamani wakati wowote kwa maelekezo ya DPP, ambaye hana budi kujiridhisha kwanza dhidi ya tuhuma hizo za ufisadi kabla ya kuruhusu sheria ichukue mkondo wake.

Wakati Wizara ya Sheria na Katiba ikitoa taarifa rasmi ya kuwasilishwa majalada yote ya watuhumiwa kwa DPP, Feleshi alilithibitishia gazeti hili jana kwamba tayari ameanza kuyachambua majalada hayo.

"Kila jalada linalokuja lazima nilisome, nilipitie kwa umakini... ndiyo utaratibu huo, hatupindishi sheria, lakini hadi sasa (jana) siko katika nafasi ya kueleza idadi ya majalada ambayo yamekuja," alifafanua DPP Feleshi.

Feleshi, ambaye ni mmoja wa watendaji serikalini wasio na urasimu wa kutoa habari, alisema hakuna mtu atapona au kuonewa katika mchakato huo.

"Hakuna namna ya mtu kuweza kupona au kuonewa, lazima nifanye Legal Analysis (uchambuzi wa kisheria) kwanza, cha msingi usiulize majalada mangapi, niulize afya yangu tu, niombe uzima tu, kila kitu utaona kitakavyokwenda," alisema DPP Feleshi.

Feleshi alisisitiza kuwa jambo kubwa na la msingi analoomba ni kuwa na afya njema kwani ana uhakika wa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria bila kupindisha.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, aliliambia gazeti hili kwamba polisi sasa inamsikiliza mkuu huyo wa mashitaka.

Kamishna Manumba alisema DPP ndiyo kiongozi wa kazi hiyo atakolosema polisi itafanya kwa mujibu wa taratibu.

"Hivi sasa kiongozi wetu ni DPP, atakachosema polisi tutafanya, kazi hii inahusisha taasisi nyingi hivyo mkurugenzi wa mashitaka ndiyo kiongozi wetu," alisisitiza Kamishna Manumba.

Wakati vigogo hao kutoka ofisi ya DPP na Polisi wakitoa misimamo hiyo, taarifa nyingine kutoka wizara hiyo ya sheria na Katiba iliyotolewa jana mchana na msemaji wake, Omega Ngole, ilisema timu ya rais imetimiza maelekezo yote ya mkuu wa nchi.

Timu ilisema kiasi cha fedha cha Sh69.3 bilioni alichotaja rais hakijaongezeka hadi kufikia Oktoba 31 na majalada yote ya kesi yameshawasilishwa kwa DPP.

"Timu inapenda kuarifu umma kuwa maelekezo yote mawili yametekelezwa. Kiasi cha fedha kilichorejeshwa hadi mwishoni mwa Ijumaa (Oktoba 31,2008) ni kilekile kilichotajwa na Mheshimiwa Rais, yaani sh 69.3 bilioni. Aidha, majalada ya kesi yamewasilishwa kwa DPP kwa ajili ya kuyafanyia kazi kama ilivyoelekezwa," alifafanua Ngole.

Akihutubia taifa Ijumaa, Rais Kikwete alisema ameagiza timu yake kwamba wamiliki wa makampuni 13 ambayo yalichota sh 90.3 bilioni na kisha yakashindwa kurejesha fedha zilizobaki, majalada yao yapelekwe kwa DPP ambaye kikatiba ndiye mwenye mamlaka ya kuandaa taratibu za kufungua mashitaka.

Hata hivyo, kauli hiyo bado ilionekana kupingwa na baadhi ya Watanzania wa kada mbalimbali ambao walisema wana imani na wanamuunga mkono Rais Kikwete, lakini wakataka mashitaka yasiwe kwa baadhi ya watuhumiwa, bali kwa wote walioiba.

Lakini, duru nyingine zinadai kuwa uamuzi huo huenda ukawa ni mbinu ya kuwatega mafisadi hao ili warejeshe fedha wote ili kiwe kidhibiti cha kuburuza nacho mahakamani kwa urahisi.

Ufisadi wa EPA ulibainika katika hesabu za BoT za mwaka 2005/06, baada ya ukaguzi wa kampuni ya Deloitte&Touche ya Afrika Kusini, ambayo ilisitishwa ghafla na Benki Kuu (BoT) kufanya kazi bila sababu za msingi baada ya kubaini Sh40 bilioni zilizochotwa na kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.

Hata hivyo, mwaka jana serikali ilimwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutafuta kampuni ya kimataifa ya kufanya tena ukaguzi.

Ofisi ya CAG iliteua kampuni ya kimataifa ya Ernst&Young, ambayo ilibaini ufisadi huo wa Sh133 bilioni, ambazo zilichotwa na makampuni 22.

Makampuni 13 yalijichotea sh 90.3 bilioni, ni pamoja na Bencon International LTD of Tanzania, Vb & Associates LTD of Tanzania, Bina Resorts LTD of Tanzania, Venus Hotel LTD of Tanzania, Njake Hotel &Tours LTD, Maltan Mining LTD ya Tanzania.

Mengine ni Money Planners & Consultants, Bora Hotels & Apartment LTD, B.V Holdings LTD, Ndovu Soaps LTD, Navy Cut Tobacco (T) LTD, Changanyikeni Residential Complex LTD na Kagoda Agriculture LTD.

Kwa upande wa makampuni tisa yaliyochota Sh42.6 bilioni yanasubiri uchunguzi zaidi unaofanywa kwa kuhusishwa serikali za nchi nyingine baada ya hatua za awali kutotoa majibu mazuri.

Makampuni yaliyo kwenye sakata hilo ni G&T International LTD, Excellent Services LTD, Mibale Farm, Liquidity Service LTD, Clayton Marketing LTD, M/S Rashtas (T) LTD, Malegesi Law Chambers (Advocates), Kiloma and Brothers na KARNEL LtD.

Kumbukumbu ya makampuni mengine mawili- Rashtas (T) na G&T International LTD, pamoja na nyaraka za usajili kwa Msajili wa Majina ya Makampuni na Biashara (BRELA), hazikuweza kupatikana.

Kufikia mwaka 1999 deni katika EPA lilifikia dola 623 milioni, ambazo kati ya hizo dola 325 milioni zilikuwa ni deni la msingi na dola 298 ni riba na baadaye deni likaongezeka hadi kufikia dola 677 milioni.

Hata hivyo, chini ya Mpango wa Kununua Madeni (Debt Buy Back Scheme) wa mwaka 1994 kati ya serikali na Benki ya Dunia (WB), waliokuwa wanaidai BoT waliombwa wakubali kulipwa sehemu tu ya fedha wanazodai. Wapo waliokubali na wengine kukataa na kuongeza hadi mwaka 2004 taarifa zinaonyesha jumla ya dola 228 zililipwa chini ya mpango huo.

EPA ni akaunti ya madeni ambayo ilitumika wakati wa Mfumo wa Ujamaa, ambayo akaunti yake ilikuwa katika iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) chini ya usimamizi wa BoT.

Mwaka 1985, EPA ilihamishiwa moja kwa moja BoT, na ndipo mwaka juzi kulipoibuka utata wa tuhuma za ufisadi katika akaunti hiyo kwa mahesabu ya mwaka 2005/06, ambayo utata huo ulisababisha Ernst&Young kufanya ukaguzi kuanzia Septemba sita na kukabidhi ripoti yake kwa CAG mapema Desemba mwaka jana