Thursday, October 16, 2008

Shilowa ana chama kipya Afrika Kusini


Wakati mgawanyiko katika chama hicho ulipojitokeza kwa mara ya kwanza, Mosiuoa Lekota, ambaye alikuwa ni waziri wa ulinzi, aligadhabishwa na viongozi ambao sasa ndio wakuu wa chama cha ANC.

Siku saba baada ya hayo, ameweza kutulia. Kundi hili jipya, ambalo bado halijafahamika, lina nia ya kuonyesha kwamba ni chama cha kisiasa ambacho kitaaminika, sio tu mkusanyiko wa wanasiasa walioshindwa vibaya mno.

Mbhazima Shilowa alijiuzulu kama kiongozi wa eneo tajiri zaidi nchini Afrika Kusini la Gauteng, ikiwa ni hatua ya kupinga kuondolewa mamlakani kwa Thabo Mbeki.

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Johannesburg, alithibitisha kwamba anakihama pia chama cha ANC.

Bw Shilowa sasa atashirikiana na Bw Lekota katika kuandaa mkutano wa kitaifa, tarehe 2 mwezi Novemba, chini ya maudhui ''Katika hali ya Kuitetea Demokrasia Yetu''.

Bw Shilowa alisema chama kipya kitajadili mabadiliko ya katiba, na kutokana na yale yaliyompata yaliyompata Thabi Mbeki akiwa rais wa Afrika Kusini, kuamua kama itafaa rais kuchaguliwa na raia moja kwa moja.

Kufikia sasa, Bw Mbeki hajazungumza lolote kuhusiana na chama kipya kilichoanzishwa na rafiki zake.

Wednesday, October 15, 2008

Ripoti Yasubiriwa Kenya Juu ya Ukabila


Viongozi wa serikali ya umoja nchini Kenya watapokea ripoti iliyochunguza ghasia za kikabila mapema mwaka huu baada ya matokeo ya uchaguzi kupingwa.

Tume iliyopewa kazi hiyo ilitakiwa kuchunguza namna vyama vya siasa pamoja na vikosi vya usalama vilivyojihusisha katika ghasia hizo.

Mwandishi wa BBC nchini Kenya Peter Greste amesema mgawanyiko uliotokea baada ya uchaguzi wa mwezi Disemba mwaka jana umekuwa wa kikabila na Kenya ilikuwa ikielekea katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Zaidi ya watu 1,500 waliuawa na wengine wanaofikia 300,000 walilazimika kuzihama nyumba zao.

Baada ya usuluhishi wa kimataifa, Rais Mwai Kibaki na aliyekuwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga walitiliana saini makubaliano ya kugawana madaraka mwezi wa Februari na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na Bwana Odinga akawa Waziri Mkuu.

Jaji Philip Waki aliongoza tume ya uchunguzi iliyoteuliwa kufuatia mapendekezo ya jopo la wasuluhishi la Umoja wa Mataifa walioongozwa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan.

Jopo hilo liliwasilisha ripoti yao kwa Bwana Kibaki na Bwana Odinga.

Siku ya Jumanne baraza la mawaziri la Kenya lilisema litatekeleza mapendekezo ya tume nyingine iliyochunguza wizi wa kura uliojitokeza, tume iliyotoa mapendekezo ya kubadilishwa Tume ya uchaguzi.


Msemaji wa aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, amesema Bwana Thabo Mbeki ana matumaini makubwa ya kuokoa mazungumzo yaliyokwama ya kugawana madaraka nchini Zimbabwe.

Msemaji huyo amesema wana hakika watafanikiwa kumaliza suala hilo, bila kujali muda utakaotumika kulitatua.

Mazungumzo ya kugawana madaraka yalikwama baada ya Rais Robert Mugabe mwishoni mwa wiki kuwateua katika wizara nyeti mawaziri kutoka chama chake cha Zanu-PF.

Leo hii Bwana Mbeki alifanya mazungumzo na viongozi wakuu wa Zimbabwe kabla Bunge halijakutana kwa mara ya kwanza tangu wabunge walipoapishwa.

Bunge lenye wabunge wengi kutoka chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC)linatazamiwa kujadiliana suala la kuifanyia marekebisho katiba, ili kumuwezesha kiongozi wa upinzani Bwana Morgan Tsvangirai awe Waziri Mkuu ikiwa ni moja ya masharti muhimu chini ya makubaliano.

Hata hivyo Bwana Tsvangirai ametishia kujiondoa katika mazungumzo hayo baada ya serikali kutangaza wizara muhimu siku ya Jumamosi ikiwemo ziara ya ulinzi, mambo ya ndani, mambo ya nje na sheria kwa chama cha Zanu-PF.

Bwana Tsvangirai anataka nafasi zote za mawaziri zipitiwe upya katika mazungumzo na Bwana Mbeki aliyesimamia mapatano hayo mwezi uliopita, lakini chama cha Zanu-PF kimesema nafasi moja tu ya wizara ya fedha ndio inaweza kujadiliwa.

Makubwa Hayo!!


Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Uyole, Dk. Catherine Madata (katikati) akimwonesha Rais Jakaya Kikwete na Mkewe Salma Kikwete mbegu mpya ya mahindi iliyo buniwa na kuzalishwa na kituo hicho wakati Rais lipotembelea kituo hicho juzi.

Piga!! Mpe Jiwe!! Huyooooo!!!....


Rais wa Chama cha Waalimu Tanzania (CWT, Gratias Mukoba akikwepa mawe kutoka kwa waalimu waliojawa na jazba akikimbilia gari la polisi , mkutano wa maandalizi ya mgomo ulivunjika, Makakama Kuu Divisheni ya Kazi ilizuia mgomo wa walimu.

POLISI jana walilazimika kutumia risasi za moto kutawanya walimu waliokuwa wakiwashambulia viongozi wa chama chao, CWT, waliotaka kuwapa taarifa kuwa mgomo wao umezuiwa na Mahakama Kuu, na badala yake wakasema watatekeleza azma yao ya kugoma kuanzia leo.

"Bora tufe kwa risasi tukaepukana na shida tunazoendelea kuzipata kuliko kuendelea kuishi maisha haya," alisema mwalimu mmoja kwenye mkutano huo ulioanza salama kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, lakini ukavunjika baada ya taarifa hiyo.

"Huu ndio wakati wa kufa tukitafuta haki zetu kwa kuwa tumechoka. Hakuna cha wito tena kwa kuwa hii ni kazi kama nyingine."

"Unajua bwana, hii serikali ina watu wanaotaka kujifanya miungu watu. Sisi tunaanza mgomo kwa aina yoyote ile iwe wa kugoma kuingia darasani au hata kama tutaingia darasani hatutafundisha na kama tukifundisha tutafundisha chini ya kiwango," alisikika mmoja wa walimu hao.

Vurugu, kelele, nyimbo za kulaani, mawe na chupa zilirushwa baada ya rais huyo wa CWT, Gratian Mukoba, kutoa tamko lililoelezea kusitishwa kwa mgomo wa walimu uliokuwa uanze leo nchi nzima kuishinikiza serikali kuwalipa walimu haki zao.

Walimu wanasema kuwa, wanaidai serikali zaidi ya Sh23 bilioni, zikiwa ni malimbikizo ya posho zao mbalimbali, fedha za nauli na pia kudai kupandishwa madaraja na haki nyingine, ambazo serikali imeeleza kuwa zitalipwa na kutekelezwa baada ya kumalizika kwa zoezi la uhakiki wa walimu.


Tuesday, October 14, 2008

Nyerere Day


Leo hii mwana GATUNDU anaungana na wanajamii wote wa Tanzania kuadhimisha miaka 9 tangu atutoke baba wetu wa taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

Tuesday, October 7, 2008

Lori Laua Watano

WATU watano akiwemo mume na wake zake wawili, wamekufa papo hapo na wengine 10 kujeruhiwa baada ya basi dogo walilokuwa wakisafaria kutoka Sirari kwenda mjini Musoma kugongwa na roli la mafuta, ajali ambayo iliwaunganisha kwa muda wagombea ubunge wa vyama vya CCM na Chadema.

Ajali hiyo ilihusisha magari namba T 808 AHU Toyota Hiace mali ya Elizabeth Pebahati, ambalo lilikuwa na abiria 15 na lori aina ya Mercedes Benz lenye namba za usajili KAZ 821 Z lililokuwa na tela namba ZC 7367 ambalo ni mali ya Kampuni ya Primefuels Liquid Transport ya nchini Kenya.

Watu watano waliokuwa wamekaa kiti cha nyuma, akiwemo mwanamume mmoja na wake zake wawili walifariki wakati wengine 10 wamejeruhiwa. Waliokufa walitambuliwa kuwa ni Gati Manyinyi, 60, aliyekuwa na wake zake wawili Msogoro Gati, 55, na Nyanoko Gati, 40, wakati maiti za watu wengine wawili bado hajizatambuliwa.

Majeruhi waliolazwa katika hospitali ya wilaya ni Marwa Mwita (46), Mwita Ndimi (25),Welema Gati (31) ambaye ni mke wa tatu wa Gati Manyinyi.

Wengine waliojeruhiwa ikiwa ni pamoja na mtu mmoja ambaye hajatambulika jina lake ni Victoria Ogeli (32), Orango Ogeli(51), Moyi Marwa Masero(23), Moris Michael (33) pamoja na Dany Nyamongo (29).

Tukio la kuokoa majeruhi na kutoa maiti kwenye gari hilo lilichukua takriban saa mbili na hivyo liliwapa muda wagombea ubunge wa CCM na Chadema kuungana na wananchi wengine kusaidia zoezi hilo.

Wakati fulani wagombea hao, Christopher Kangoye wa CCM na Charles Mwera wa Chadema, walibeba miili ya watu hao kwa pamoja na kuipandisha kwenye gari.

Jasinta Mwikali, ambaye ni mkazi wa Nairobi nchini Kenya, alisema: “Tulipofika eneo hilo dereva alisimama na kuanza kuzungumza na dereva mwenzake wa Hiace nyingine wakiulizana iwapo mbele kuna trafiki, lakini ghafla tuliona roli hilo likija kwa kasi nyuma yetu.

"Mbele pia kulikuwa na roli jingine likija kasi ndipo dereva alipoondoa gari lakini gari letu liligongwa kwa nyuma."

Walisema ilikuwa ni kazi ngumu kuondoa watu waliokuwa kwenye Hiace kutokana na lori hilo kupanda juu yake na ililazimika kutumia lori jingine la mafuta kuivuta Hiace hiyo ambayo ilitoka ikiwa vipande na maiti moja na maiti nyingine kukandamizwa na tairi la roli hilo.

Dereva wa roli hilo ambaye hajajulikana jina lake amekimbia, wakati dereva wa Hiace hiyo, Mwijuma Abasi pamoja na kondakta wake, Robert Daudi walisalimika na walikuwepo katika eneo hilo la ajali wakisaidia uokoaji.

Happy Birthday JK

Wana-Gatundu wote ulimwenguni wanamtakia kheri ya kuzaliwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye alizaliwa tarehe kama ya leo.
Happy Birthday JK

Monday, October 6, 2008

Padri Ataka Prof. Kapuya Ajiuzulu

PADRI wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mkokola, Father Winnefrid Dinno amesema Rais Jakaya Kikwete alitumia busara kumtuma Profesa Juma Kapuya kuja Tabora kujionea vifo vya watoto 19 vilivyotokea kwenye jengo la taasisi iliyo chini ya wizara yake, ili waziri huyo ajipime na baadaye kujiwajibisha.

Akihubiri kwenye ibada maalum ya kuwaombea waliofariki, Fr Dinno alisema Prof Kapuya anatakiwa ajiuzulu kwa kuwa anajua kuwa jengo lililoua watoto hao liko chini ya wizara yake na kwamba, alikuwa anajua kuwa kulikuwa na matukio mawili kama hayo kwenye jengo hilo, ingawa hayakuua.

"Alinyamaza kimya mpaka tukio hili limekuwa kubwa kiasi ambacho kimekuwa ni kitendawili kisicho na mteguaji," alisema Fr Dinno alirejea matukio ya mwaka 2006 na 2007 ambayo yalisababisha watoto kadhaa kuzirai baada ya kutokea hitilafu kama hiyo kwenye ukumbi wa Bubbles.

"Waziri wa Russia alijiuzulu kwa vifo tena vya watu wazima, iweje Kapuya asiachie ngazi kutokana na vifo vya watoto 19 ambao ni nguvu kazi ya kesho," alihoji huku akionyesha kutoridhika na juhudi ambazo serikali inadai inazifanya kujua chanzo.

"Kushikilia wahusika hakusaidii kwani bado watu muhimu hawajaachia ngazi. Waachie ngazi kwanza ndio haki itatendeka, vinginevyo tutaletewa ripoti ambayo hata mtu ambaye hajasoma hawezi kukubaliana nayo."

Fr Dinno alisema rais ana busara sana kwa kuwa alijua kwamba mhusika mkuu katika vifo hivyo ni waziri mwenye mamlaka na jengo hilo ndiyo maana alimtuma kumwakilisha kuhudhuria mazishi hayo ili aweze kujipima yeye mwenyewe na kuachia ngazi.

Fr. Dinno alisema mbali na hayo, viongozi hao waliwaambia wafiwa kwamba vifo hivyo ni vya kawaida kwani kuna mtu mmoja mkoani Arusha aliwahi kununua kila kitu, lakini alipokuwa akila mfupa ulimkwama na kupoteza maisha na kwamba ndugu zake hakupewa chochote.

"Kauli za namna hiyo ni za kejeli na hazifai kwa watu ambao wana majonzi mazito kama hayo," alisema Padri huyo.

"Hawa ni viongozi wanaowakilisha watu na watu wenyewe ndio hao wanaowatolea maneno ya kejeli na katika majonzi mazito kama haya.

"Nyie viongozi ni bora mje mtubu kabla ili mtakapojiuzulu jamii iwaone kwamba kejeli mlizozitoa hamkudhamiria mkiwa kama viongozi mliotumwa na rais."

Mazungumzo ya Muungano Yakwama


Mazungumzo kati ya rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na waziri mkuu mpya Morgan Tsvangirai yameshindwa kufikia muafaka juu ya baraza la pamoja.

Viongozi hao wawili walitia saini makubaliano ya kugawana madaraka takriban wiki tatu baada ya kufanyika uchaguzi wenye utata nchini humo mwezi Juni.

Katika makubaliano hayo iliamuliwa kuwa Bw Mugabe ambaye amekaa madarakani kwa miongo mitatu atabaki kuwa rais huku Bw Tsvangirai akiwa waziri mkuu.

Pande zote mbili zimekubaliana kukutana mapema wiki ijayo ili kuanza upya mazungumzo.

Msemaji wa chama cha Bw Tsvangirai cha MDC amesema majadiliano hayo yalikuwa ya wazi lakini bado yamekwama.

Msemaji wa Bw Mugabe George Charamba, amesema tofauti zilizokuwepo ni nani apewe uongozi wa uwaziri wa fedha na waziri wa mambo ya ndani.

Chameleon Ajirusha Ghorofani

MSANII maarufu wa Uganda, Jose Chameleon amejirusha kutoka ghorofa ya tatu ya Hoteli ya Impala mjini Arusha na kusababisha kuumia vibaya ikiwa ni pamoja na kuvunjika miguu yote.

Chameleon ambaye amekuwa akitamba na nyimbo za ‘Jamila’, ‘Mama Mia’ na nyingine alijirusha kutoka chumbani kwake katika ghorofa ya tatu ya hoteli hiyo alfajiri ya saa 11 kuamkia juzi.

Imeelezwa msanii huyo alishituka akiwa chini amevunjika miguu hiyo na walinzi walikimbilia eneo aliloangukia baada ya kusikia kishindo na kumkuta akiwa hawezi kuinuka.

Hata hivyo haikueleweka kilichomfanya msanii huyo ajirushe, baadaye wenyeji wake ambao ni Clouds FM waliokuwa wamemualika kwa ajili ya shughuli ya Fiesta ya Tanga juzi walibidi kufanya utaratibu wa kumpeleka hospitali.

Lakini baadaye walitakiwa kutomtibu na baba yake aliagiza ndege ambayo ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa KIA na kumbeba na kumpeleka Uganda ambako amelazwa katika hospitali moja ya nchini humo akipata matibabu.

Kuumia kwa msanii huyo kulisababisha ashindwe kufanya shoo katika tamasha la Fiesta ambako kulikuwa na wasanii wengi wa Tanzania na yeye ndiye alikuwa mgeni aliyetakiwa kuongoza shoo hiyo.

Fiesta ya Tanga ilifanyika juzi Jumamosi na wasanii kadhaa walifanya vizuri huku idadi kubwa ya mashabiki wakiwa wamejitokeza katika shoo hiyo ya ufunguzi wa tamasha hilo maarufu zaidi nchini.

 

Friday, October 3, 2008

Mwangura Afikishwa Mahakamani

Afisa wa shirika la kuhudumia mabaharia mashariki mwa Afrika, Bw Andrew Mwangura, amefikishwa mahakamani na kushitakiwa kwa kutoa habari za kutekwa nyara kwa meli ya Ukraine, yenye vifaru 33 vya kivita.

Bw Mwangura ameshitakiwa kwa madai ya kutoa habari zilizokuwa na lengo la kusababisha fujo na uhasama nchini.

Afisa huyo ambae amekuwa akitoa vidokezo kuhusu meli ya Ukraine yenye silaha za kivita pia alishitakiwa kwa kuwa na bangi.

Hata hivyo, Bw Mwangura, ambae alikamatwa jana usiku, anadai maisha yake yamo hatarini.

Pamoja Daima


Mtandao wa simu za mikononi wa Vodacom, hivi majuzi umeanzisha huduma mpya inayoitwa CHIZIKA na Vodacom, ambapo unawapa fursa wateja wake kupiga simu kwanzia saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni kwa shilingi 1500/= tu za kitanzania.

Kujiunga na huduma hii unatakiwa kuhakikisha kuwa una salio la kutosha yaani Tsh 1500/- au zaidi, kisha unapiga namba *147#, baada ya apo utakuwa umejiunga na huduma hiyo ya chizika na vodacom.

Pamoja Daima

MDAU

INTERNET BURE!!!!!!!!!!!!
Mdau Edgar (Mtaalamu wa M-Pesa) akiwa ana zuru blog ya Gatundu na kutuma report yake huku akitumia Mtandao wa Vodacom kupitia kifaa kinachoitwa 3G USB Modem kinachopatikana VodaCom pekee.

Huduma hii Mdau huyu anaipata bure na inapatikana katika ofisi za Vodacom Mlimani City, yaani internet surfing ni bure!!.

Ufaransa Waingilia Suala la EPA

MKATABA wa ukaguzi wa deni la mamilioni ya shilingi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani Benki Kuu ya Tanzania (BoT), umekamilika na Kampuni ya Lazard iliyoteuliwa kufanya ukaguzi huo kuanzia mapema mwezi huu.

Uhakiki huo wa Kampuni ya Lazard ya Ufaransa, uunafanyika wakati BoT imepoteza zaidi ya Sh133 bilioni katika akaunti hiyo zilizotolewa kwa mafisadi katika mazingira ya kutatanisha.

Taarifa kutoka BoT ambazo zilithibitishwa na Gavana wa benki hiyo, Profesa Benno Ndulu, zilisema kuwa mkataba huo uko tayari na Lazard inatarajiwa kuanza kazi wakati wowote kuanzia sasa.

Profesa Ndulu alisema kukamilika kwa mkataba huo kunatokana na mchakato wa muda mrefu uliohusisha BoT na Benki ya Dunia (WB).

"Ndiyo, tumemaliza kukamilisha mkataba, Lazard inatarajiwa kuanza kazi rasmi mwezi huu," alithibitisha gavana Profesa Ndulu.

Profesa Ndulu alifafanua kwamba, katika mkataba huo Lazard pamoja na mambo mengine itaishauri BoT namna bora ya kuachana na usimamizi wa fedha za EPA.

Akiweka bayana, alisema BoT inataka kubaki katika majukumu yake ya kimsingi na kisheria, ambayo ni pamoja na ile ya Benki Kuu ya mwaka 2006.

Kuhusu muda wa ukaguzi huo, Ndulu alisema mkataba unaeleza kwamba Lazard itapaswa kufanya ukaguzi kwa kipindi cha miezi tisa.

"Jambo kubwa pamoja na mengine ni namna ambavyo wananchi yaani BoT itaachana na majukumu ya usimamizi wa fedha za EPA," aliongeza gavana Profesa Ndulu.

Alisema WB ilishiriki katika kuandaa mkataba huo kwani siku za nyuma, iliwahi kushiriki pamoja na kampuni hiyo kuisaidia BoT katika malipo ya fedha za EPA.

Gavana Ndulu aliongeza kwamba, Lazard ni kampuni ambayo awali ilifanyakazi na BoT katika mambo mbalimbali ikiwemo ushauri wa namna bora ya kuimarisha mfumo wa fedha.

Alisema uamuzi wa kuiteua Lazard unatokana na uzoefu wa kampuni hiyo ya Ufaransa, katika utendajikazi wa BoT hasa katika suala la fedha za EPA.

"Hawa Lizard si wageni ndani ya BoT, siku za nyuma waliwahi kufanyakazi nasi na waliweza kutusaidia,"alisisitiza.

Kuanza kwa ukaguzi huo itakuwa ni hatua moja mbele ya kuondoa mzigo wa usimamizi wa fedha za EPA mikononi mwa BoT.

BoT kwa mujibu wa Sheria ya mwaka 2006, inamajukumu mbalimbali ambayo ni pamoja na usimamizi wa shughuli za uchumi wa nchi na sekta ya fedha.

Kusitishwa malipo ya EPA kulifanyika mara baada ya kubainika kwa ufisadi huo baada ya ukaguzi ukufanywa na kampuni ya Ernst$Young na matokeo yake kutangazwa na serikali Januari 9, mwaka huu.

Kwa mujibu wa takwimu za serikali, deni la EPA hadi mwaka 1999 lilifikia dola za Marekani 623 milioni, ambazo kati ya hizo dola 325 milioni zilikuwa ni deni la msingi na dola 298 ni riba na baadaye likaongezeka hadi kufikia dola 677 milioni.

Hata hivyo, kulikuwa na Mpango wa Kununua Madeni (Debt Buy Back Scheme) wa mwaka 1994 kati ya serikali na WB, ambao waliokuwa wakidai BoT waliombwa wakubali kulipwa sehemu tu ya fedha wanazodai.

Katika mpango huo, wapo waliokubali na wengine kukataa na kuongeza kuwa hadi mwaka 2004 taarifa zinaonyesha jumla ya dola 228 zililipwa chini ya mpango huo.

Hata hivyo, utaratibu huo ndiyo ulileta matatizo ambayo yalibainika katika Ukaguzi wa Hesabu za BoT za mwaka 2005/06, ambao ulifanyika Agosti mwaka 2005, ulionyesha matatizo katika ulipaji wa madeni kwa utaratibu wa idhini ya kulipwa wakala wa mdai katika akaunti ya EPA.

Baada ya hapo, kulitokea hali ya kutoelewana kati ya BoT na Mkaguzi Kampuni ya Deloitte & Touche ya Afrika Kusini, aliyegundua tatizo hilo, lakini serikali iliingilia kati na Desemba 4, 2006, ilimuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhakikisha ukaguzi huo unafanyika kwa kina ambao ulifanywa na Ernst&Young na kubaini ufisadi wa zaidi ya sh 133 bilioni zililizolipwa kwa makampuni 22.

Kufuatia ufisadi huo, Januri 9 Rais Jakaya Kikwete, alitangazia umma kupitia Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo, kuhusu kutimuliwa kazi kwa aliyekuwa Gavanawa BoT, marehemu Daud Ballali na kuunda Timu Maalumu chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, kuchunguza, kukamata na kufungua mashitaka dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi huo.

EPA ni akaunti ya madeni ambayo ilitumika wakati wa Mfumo wa Ujamaa, ambayo awali ilikuwa katika iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) chini ya usimamizi wa BoT.

Mwaka 1985, EPA ilihamishiwa moja kwa moja BoT na ndipo mwaka juzi ziliibuliwa tuhuma za ufisadi katika akaunti hiyo

Kp Leo

Moshi Si Mchezo

Mfanyakazi wa Kampuni ya Bonite mjini Moshi akifanya usafi wa kupunguzia nyasi katika bustani iliyopo mzunguko wa Bonite mjini Moshi ambao unahudumiwa na kampuni hiyo alhamisi. Licha ya ukame uliopo katika mji huo lakini bado madhari ya bustani zake inavutia kutokana na kuhudumiwa vyema.

Watoto 19 Wafa Disco

Polisi katikati ya Tanzania imesema takriban watoto 19 wamekufa baada ya kutokea mkanyagano kwenye ukumbi wa Disco wakati wa sikukuu ya Idd.

Tukio hilo la kukanyagana ndani ya ukumbi wa disco limetokea katika mkoa wa Tabora kilometa 750 kaskazini magharibi mwa mji wa Dar es Salaam.

Disco hilo hilo lilikuwa limeandaliwa kama sehemu ya sherehe za Idd al-Fitr kuadhimisha kumalizika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Waliokufa katika mkasa huo ni vijana kati ya umri wa miaka 12 na 17.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Tabora Daudi Siasi, ameliambia Shirika la Utangazaji la Tanzania, kwa mujibu wa uchunguzi wa awali vijana hao 19 walikufa kutokana na kukanyagana na wengine kukosa hewa wakiwa ndani ya ukumbi wa disco.

Kamanda Siasi amesema watu kadha walitibiwa hospitalini kutokana na majeraha waliyopata.

Uchunguzi wa polisi bado unaendelea.

Tuesday, September 30, 2008

Tarime Si Shwari

Lori aina ya Mitsubishi Fuso namba T741AEK linalotumiwa na CHADEMA katika kampeni jimboni Tarime, linaonekana likiwa limevunjwa kioo cha mbele katika tukio la juzi usiku na mtu asiyefahamika.

Kongo Yajibu Shutuma za Askari Watoto

Waziri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametoa changamoto kwa ripoti iliyotolewa juu ya ongezeko la kuingiza watoto jeshini na vitendo vya ubakaji mashariki mwa nchi hiyo.

Waziri wa ulinzi, Chikez Diemu, alisema serikali inatatua matatizo hayo kwa kuwakamata washukiwa na kuwafikisha katika mahakama za kijeshi.

Ripoti iliyotolewa na shirika la kimataifa la Amnesty imesema kwa kila askari watoto wawili walioachiliwa huru, watano hurejeshwa tena katika jeshi hilo.

Mifano ya watoto hao waliotolewa mfano katika ripoti hiyo ni kutoka jimbo la Kivu kaskazini.

Ilisema baadhi ya askari hao watoto walioruhusiwa kwenda kwao walichukuliwa tena na makundi ya watu wenye silaha.

Jeshi la Kongo limekuwa likipigana na wapiganaji wanaomtii Jenerali Laurent Nkunda mashariki mwa nchi hiyo.

Mapigano hayo yamesababisha maelfu ya watu kuhama makazi yao.

Watalii Waliotekwa Waachiwa Huru


Kundi la watalii kutoka nchi za magharibi na waongozaji wao wenye uraia wa Misri waliotekwa nyara siku 10 zilizopita wameachiliwa huru.

Mateka hao 11 wakiwemo Waitaliano watano, Wajerumani watano na raia mmoja wa Romania na waongozaji wao wameripotiwa kuwa katika afya njema.

Kundi hilo lililotekwa nyara katika mji mmoja mpakani mwa Misri kwa sasa wanaelekea mjini Cairo.

Wakati wa utekaji nyara huo watu hao walizungushwa katika eneo la jangwa lisiloruhusiwa kupitwa lililosambaa maeneo ya Misri, Sudan, Libya na Chad.

Hatua ya kuachiliwa huru kwa watu hao ulitangazwa katika televisheni ya taifa ya Misri na kuthibitishwa na wizara ya mambo ya nje ya Italia.

Watekaji nyara hao walitaka Ujerumani ilipe fidia ya dola za kimarekani milioni 8.8.

Haijajulikana wazi iwapo fidia hiyo ililipwa.

Monday, September 29, 2008

Katuni Leo

17 Walipuliwa Syria


Serikali ya Syria imesema takriban watu 17 wameuawa na wengine 14 kujeruhiwa katika shambulio la bomu lililotegwa ndani ya gari nje ya mji mkuu, Damascus.

Eneo lililokusudiwa kulipuliwa bomu hilo halijajulikana lakini limelipuka karibu na msikiti mmoja wa madhehebu ya Shia na kituo kimoja cha usalama.

Mashambulio kama hayo ni nadra sana kutokea nchini humo.

Mlipuko huo unaonekana kuwa tishio kubwa kabisa kwa usalama wa taifa hilo kutokea katika kipindi cha miaka mingi iliyopita.

Waziri wa mambo ya ndani wa Syria, Jenerali Bassam Abdel Majid, ameelezea shambulio hilo kuwa la kigaidi.

Hata hivyo amekataa kusema ni nani anayehusika na shambulio hilo.

Televisheni ya Syria ilisema gari lililokuwa na mabomu yenye kilo 200 lililipuliwa karibu na kituo cha usalama cha ukaguzi wa magari katika barabara inayoelekea uwanja wa ndege nchini Syria.

Wamarekani Wawakaribia Maharamia

Meli ya kivita ya Marekani imefanya mawasiliano na meli ya Ukraine iliyokamatwa na maharamia wa kisomali wiki iliyopita iliyotia nanga karibu na bandari ya Dobyo.

Hakuna ishara zozote kuonyesha kuwa meli hiyo ya Marekani ya USS Howard inaikaribia meli ya MV Faina iliyobeba vifaru vya kivita 33 aina ya T-72.

Meli hiyo ya MV Faina ilikuwa ikielekea nchini Kenya.

Meli nyingine ya kivita ya kirusi nayo inaelekea katika eneo hilo.

Maharamia hao wameripotiwa kudai fidia ya dola za kimarekani milioni 35 ili kuiachia huru meli hiyo ya Ukraine na mabaharia wake.

Hata hivyo, serikali ya Kenya imeonyesha wasiwasi juu ya ripoti hiyo ikisema kuwa hakukuwepo na taarifa za kutaka kulipwa fidia.

Maharamia hao pia walitoa onyo dhidi ya jitihada zozote za kuokoa mabaharia na meli hiyo.

kp Leo

Denti Akamatwa na Shahada


MWANAFUNZI wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Rebu wilayani Tarime amekamatwa kwa tuhuma za kuuza shahada tano za kupigia kura ikiwemo ya kwake mwenyewe. 

Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Polisi cha Oparesheni Maalumu, Naibu Kamishna wa Polisi, Bw. Venance Tossi katika mkutano na waandishi wa habari ilisema mwanafunzi huyo aliyejulikana kwa jina la Mahemba Daudi (18) alikamatwa saa nne asubuhi alipokwenda kuuza shahada hizo katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani Tarime. 

Bw. Tossi alisema baada ya vijana wa CCM kumkamata, walimfikisha kituo cha Polisi ambako alifunguliwa shitaka la jinai la kutaka kuuza shahada kinyume cha sheria. 

"Tumemhoji mtuhumiwa kujua shahada zimemfikiaje, mpaka sasa nimeshatuma timu ya wapelelezi kufuatilia ili tujue nani walimtuma au kama zimeibwa,” alisema Kamanda Tossi na kuongeza kwamba "Endapo itabainika, basi yeye pamoja na watakaohusishwa na tukio hilo watapelekwa haraka mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.” 

Alipoulizwa kuwa kijana huyo ni mfuasi wa chama gani, Kamanda Tossi alijibu kuwa kazi ya Jeshi la Polisi si kujua hilo bali kwa vile shahada si mali ya chama chochote, ila cha muhimu ni kuwakamata watu wote wanaofanya biashara hiyo ya kuziuza kwani ni kosa la jinai. 

“Anayeuza shahada na anayenunua wote wanafanya kosa la jinai, wakikamatwa watachukuliwa hatua za kisheria, hivyo tunatoa mwito kwa wananchi kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi endapo watamwona yeyote akiuza shahada,” alisema Kamanda Tossi. 

Kamanda Tossi alisema kabla ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilikuwa halijapata taarifa kutoka chama chochote kulalamikia biashara ya uuzaji shahada. 


Uchunguzi Kesi ya Ufisadi Yaendelea Vizuri


MWEZI mmoja baada ya serikali kutangaza uchunguzi wa Jeshi la polisi kuona kama kampuni ya ufuaji umeme ya Richmond (LLC) ilighushi nyaraka kupata zabuni ya kufua umeme wa dharura, tayari baadhi ya watu wenye uhusiano na kampuni hiyo wamehojiwa.

Uchunguzi huo ni sehemu ya hatua za serikali kutekeleza maazimio 23 ya Bunge la Jamhuri ya Muungano. Azimio la 17 kati ya hayo 23 linataka mhimili huo wa dola uchunguze kuona kama LLC ilighushi nyaraka kupata zabuni hiyo ya mkataba wa Sh179 bilioni, ambao ulisainiwa Juni 23, 2006 .

Kamishna Manumba alisema polisi inafanya uchunguzi wa kina wa kijinai kwa ajili ya kupeleka kesi mahakamani.

"Uchunguzi wetu ni wa kina," alisema Manumba. "Tunafanya uchunguzi kwa ajili ya kesi, hivyo lazima tupate taarifa za kutosha.

"Hatufanyi uchunguzi wa kisiasa. Uliofanyika awali ulikuwa wa kisiasa tofauti na wa kwetu. Huu ni wa kijinai kwa ajili ya kesi mahakamani."

Alipoulizwa kuhusu baadhi ya watu kuhojiwa, alijibu: "Sasa, huwezi kuzungumzia hadharani uchunguzi unaondelea, kumbuka huu bado ni uchunguzi."

Alipoulizwa kama polisi wake wameenda Marekani kufanya uchunguzi kutokana na LLC kuhusishwa na watu kutoka nchi hiyo, Kamishna Manumba alijibu: "Nafikiri sasa tukisema tutaharibu uchunguzi, elewa tunafanya uchunguzi na unakwenda vizuri."


Athumani Hamis Apelekwa Afrika ya Kusini Kwa Matibabu Zaidi

Mhariri wa Picha wa Magazezeti ya HabariLeo na HabariLeo Jumapili, Athumani Hamisi akipandishwa katika gari la wagojwa tayari kwa safarai ya uwanja wa ndege ambako alikuwa akisafirishwa kwenda nchini Afrika Kusini kwa matibabu zaidi kufuatia ajali ya gari aliyoipata mamepa mwezi huu Wilayani Kilwa. Athumani aliumia zaidi kifua na shingo alisafirishwa jana kwa ndege ya ATCL.

Sunday, September 28, 2008

Obama Amshinda McCain Kwenye Mdahalo


Maoni ya papo kwa hapo yaliyopokelewa na kituo cha televisheni cha CNN pamoja na kituo cha utafiti wa maoni cha Opinion Research Corp yameonesha Bwana Obama alipata asilimia 51 wakati Mc Cain alama zake zilikuwa asilimia 38.

Hata hivyo pande zote zimedai kupata ushindi katika mdahalo huo, huku upande wa Bwana Mc Cain ukisema mgombea wao amemudu zaidi masuala ya usalama wa taifa, wakati wasaidizi wa Bwana Obama wamedai mgombea wao amefaulu mtihani wa kuwa amiri jeshi mkuu kwa kiwango cha juu.

Bwana Obama amesema dola bilioni 700 za mipango ya kuunusuru uchumi wa Marekani ni hukumu ya mwisho kwa utawala wa chama cha Republican.

Amesema Bwana McCain alikuwa amekosea katika suala la Iraq na amemfananisha na Rais Bush. Mgombea wa chama cha Republican Seneta Mac Cain amemuelezea mpinzani wake hana uzoefu wa kuongoza.

Katika mdahalo huo hakuna aliyemuangusha mwenzake, ila maoni ya awali yanaonesha Bwana Obama amefanya vyema zaidi.

Si Kila Kiongozi ni Fisadi - JK


RAIS Jakaya Mrisho Kikwete amesema si kila kiongozi wala kila mtumishi wa umma barani Afrika ni mla rushwa ingawa amekiri kwa kiasi fulani tatizo hilo bado lipo barani humo. 

Rais alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu maswali baada ya kumaliza hotuba yake kwenye mkutano na wajumbe wa taasisi ya Foreign Policy Brain Trust ambayo ni ya wabunge wenye asili ya Afrika mjini Washington. 

"Tusijiweke katika hali ya kutengeneza mazingira ya kwamba kila jambo linaloendelea katika Afrika ni rushwa tu," alisema Rais Kikwete. 

Aliongeza kuwa: "Hatukatai kuwa ipo rushwa katika Afrika. Tunachosema ni kwamba jambo hilo linatiwa chumvi nyingi kupita kiasi". 

Kuhusu Tanzania, Rais Kikwete alisema kuwa Serikali yake inapambana kwa dhati na changamoto hiyo ya rushwa kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya Tanzania. 

"Moja ya dalili za Serikali inayokula rushwa ni kushuka kwa mapato ya Serikali au Serikali kushindwa kukusanya mapato. Mapato yetu (Tanzania) yamekuwa yakiongezeka kila mwaka tokea tulipoingia madarakani," alisema Rais Kikwete na kushangiliwa.