Tuesday, September 30, 2008

Tarime Si Shwari

Lori aina ya Mitsubishi Fuso namba T741AEK linalotumiwa na CHADEMA katika kampeni jimboni Tarime, linaonekana likiwa limevunjwa kioo cha mbele katika tukio la juzi usiku na mtu asiyefahamika.

Kongo Yajibu Shutuma za Askari Watoto

Waziri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametoa changamoto kwa ripoti iliyotolewa juu ya ongezeko la kuingiza watoto jeshini na vitendo vya ubakaji mashariki mwa nchi hiyo.

Waziri wa ulinzi, Chikez Diemu, alisema serikali inatatua matatizo hayo kwa kuwakamata washukiwa na kuwafikisha katika mahakama za kijeshi.

Ripoti iliyotolewa na shirika la kimataifa la Amnesty imesema kwa kila askari watoto wawili walioachiliwa huru, watano hurejeshwa tena katika jeshi hilo.

Mifano ya watoto hao waliotolewa mfano katika ripoti hiyo ni kutoka jimbo la Kivu kaskazini.

Ilisema baadhi ya askari hao watoto walioruhusiwa kwenda kwao walichukuliwa tena na makundi ya watu wenye silaha.

Jeshi la Kongo limekuwa likipigana na wapiganaji wanaomtii Jenerali Laurent Nkunda mashariki mwa nchi hiyo.

Mapigano hayo yamesababisha maelfu ya watu kuhama makazi yao.

Watalii Waliotekwa Waachiwa Huru


Kundi la watalii kutoka nchi za magharibi na waongozaji wao wenye uraia wa Misri waliotekwa nyara siku 10 zilizopita wameachiliwa huru.

Mateka hao 11 wakiwemo Waitaliano watano, Wajerumani watano na raia mmoja wa Romania na waongozaji wao wameripotiwa kuwa katika afya njema.

Kundi hilo lililotekwa nyara katika mji mmoja mpakani mwa Misri kwa sasa wanaelekea mjini Cairo.

Wakati wa utekaji nyara huo watu hao walizungushwa katika eneo la jangwa lisiloruhusiwa kupitwa lililosambaa maeneo ya Misri, Sudan, Libya na Chad.

Hatua ya kuachiliwa huru kwa watu hao ulitangazwa katika televisheni ya taifa ya Misri na kuthibitishwa na wizara ya mambo ya nje ya Italia.

Watekaji nyara hao walitaka Ujerumani ilipe fidia ya dola za kimarekani milioni 8.8.

Haijajulikana wazi iwapo fidia hiyo ililipwa.

Monday, September 29, 2008

Katuni Leo

17 Walipuliwa Syria


Serikali ya Syria imesema takriban watu 17 wameuawa na wengine 14 kujeruhiwa katika shambulio la bomu lililotegwa ndani ya gari nje ya mji mkuu, Damascus.

Eneo lililokusudiwa kulipuliwa bomu hilo halijajulikana lakini limelipuka karibu na msikiti mmoja wa madhehebu ya Shia na kituo kimoja cha usalama.

Mashambulio kama hayo ni nadra sana kutokea nchini humo.

Mlipuko huo unaonekana kuwa tishio kubwa kabisa kwa usalama wa taifa hilo kutokea katika kipindi cha miaka mingi iliyopita.

Waziri wa mambo ya ndani wa Syria, Jenerali Bassam Abdel Majid, ameelezea shambulio hilo kuwa la kigaidi.

Hata hivyo amekataa kusema ni nani anayehusika na shambulio hilo.

Televisheni ya Syria ilisema gari lililokuwa na mabomu yenye kilo 200 lililipuliwa karibu na kituo cha usalama cha ukaguzi wa magari katika barabara inayoelekea uwanja wa ndege nchini Syria.

Wamarekani Wawakaribia Maharamia

Meli ya kivita ya Marekani imefanya mawasiliano na meli ya Ukraine iliyokamatwa na maharamia wa kisomali wiki iliyopita iliyotia nanga karibu na bandari ya Dobyo.

Hakuna ishara zozote kuonyesha kuwa meli hiyo ya Marekani ya USS Howard inaikaribia meli ya MV Faina iliyobeba vifaru vya kivita 33 aina ya T-72.

Meli hiyo ya MV Faina ilikuwa ikielekea nchini Kenya.

Meli nyingine ya kivita ya kirusi nayo inaelekea katika eneo hilo.

Maharamia hao wameripotiwa kudai fidia ya dola za kimarekani milioni 35 ili kuiachia huru meli hiyo ya Ukraine na mabaharia wake.

Hata hivyo, serikali ya Kenya imeonyesha wasiwasi juu ya ripoti hiyo ikisema kuwa hakukuwepo na taarifa za kutaka kulipwa fidia.

Maharamia hao pia walitoa onyo dhidi ya jitihada zozote za kuokoa mabaharia na meli hiyo.

kp Leo

Denti Akamatwa na Shahada


MWANAFUNZI wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Rebu wilayani Tarime amekamatwa kwa tuhuma za kuuza shahada tano za kupigia kura ikiwemo ya kwake mwenyewe. 

Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Kitengo cha Polisi cha Oparesheni Maalumu, Naibu Kamishna wa Polisi, Bw. Venance Tossi katika mkutano na waandishi wa habari ilisema mwanafunzi huyo aliyejulikana kwa jina la Mahemba Daudi (18) alikamatwa saa nne asubuhi alipokwenda kuuza shahada hizo katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani Tarime. 

Bw. Tossi alisema baada ya vijana wa CCM kumkamata, walimfikisha kituo cha Polisi ambako alifunguliwa shitaka la jinai la kutaka kuuza shahada kinyume cha sheria. 

"Tumemhoji mtuhumiwa kujua shahada zimemfikiaje, mpaka sasa nimeshatuma timu ya wapelelezi kufuatilia ili tujue nani walimtuma au kama zimeibwa,” alisema Kamanda Tossi na kuongeza kwamba "Endapo itabainika, basi yeye pamoja na watakaohusishwa na tukio hilo watapelekwa haraka mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.” 

Alipoulizwa kuwa kijana huyo ni mfuasi wa chama gani, Kamanda Tossi alijibu kuwa kazi ya Jeshi la Polisi si kujua hilo bali kwa vile shahada si mali ya chama chochote, ila cha muhimu ni kuwakamata watu wote wanaofanya biashara hiyo ya kuziuza kwani ni kosa la jinai. 

“Anayeuza shahada na anayenunua wote wanafanya kosa la jinai, wakikamatwa watachukuliwa hatua za kisheria, hivyo tunatoa mwito kwa wananchi kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi endapo watamwona yeyote akiuza shahada,” alisema Kamanda Tossi. 

Kamanda Tossi alisema kabla ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilikuwa halijapata taarifa kutoka chama chochote kulalamikia biashara ya uuzaji shahada. 


Uchunguzi Kesi ya Ufisadi Yaendelea Vizuri


MWEZI mmoja baada ya serikali kutangaza uchunguzi wa Jeshi la polisi kuona kama kampuni ya ufuaji umeme ya Richmond (LLC) ilighushi nyaraka kupata zabuni ya kufua umeme wa dharura, tayari baadhi ya watu wenye uhusiano na kampuni hiyo wamehojiwa.

Uchunguzi huo ni sehemu ya hatua za serikali kutekeleza maazimio 23 ya Bunge la Jamhuri ya Muungano. Azimio la 17 kati ya hayo 23 linataka mhimili huo wa dola uchunguze kuona kama LLC ilighushi nyaraka kupata zabuni hiyo ya mkataba wa Sh179 bilioni, ambao ulisainiwa Juni 23, 2006 .

Kamishna Manumba alisema polisi inafanya uchunguzi wa kina wa kijinai kwa ajili ya kupeleka kesi mahakamani.

"Uchunguzi wetu ni wa kina," alisema Manumba. "Tunafanya uchunguzi kwa ajili ya kesi, hivyo lazima tupate taarifa za kutosha.

"Hatufanyi uchunguzi wa kisiasa. Uliofanyika awali ulikuwa wa kisiasa tofauti na wa kwetu. Huu ni wa kijinai kwa ajili ya kesi mahakamani."

Alipoulizwa kuhusu baadhi ya watu kuhojiwa, alijibu: "Sasa, huwezi kuzungumzia hadharani uchunguzi unaondelea, kumbuka huu bado ni uchunguzi."

Alipoulizwa kama polisi wake wameenda Marekani kufanya uchunguzi kutokana na LLC kuhusishwa na watu kutoka nchi hiyo, Kamishna Manumba alijibu: "Nafikiri sasa tukisema tutaharibu uchunguzi, elewa tunafanya uchunguzi na unakwenda vizuri."


Athumani Hamis Apelekwa Afrika ya Kusini Kwa Matibabu Zaidi

Mhariri wa Picha wa Magazezeti ya HabariLeo na HabariLeo Jumapili, Athumani Hamisi akipandishwa katika gari la wagojwa tayari kwa safarai ya uwanja wa ndege ambako alikuwa akisafirishwa kwenda nchini Afrika Kusini kwa matibabu zaidi kufuatia ajali ya gari aliyoipata mamepa mwezi huu Wilayani Kilwa. Athumani aliumia zaidi kifua na shingo alisafirishwa jana kwa ndege ya ATCL.

Sunday, September 28, 2008

Obama Amshinda McCain Kwenye Mdahalo


Maoni ya papo kwa hapo yaliyopokelewa na kituo cha televisheni cha CNN pamoja na kituo cha utafiti wa maoni cha Opinion Research Corp yameonesha Bwana Obama alipata asilimia 51 wakati Mc Cain alama zake zilikuwa asilimia 38.

Hata hivyo pande zote zimedai kupata ushindi katika mdahalo huo, huku upande wa Bwana Mc Cain ukisema mgombea wao amemudu zaidi masuala ya usalama wa taifa, wakati wasaidizi wa Bwana Obama wamedai mgombea wao amefaulu mtihani wa kuwa amiri jeshi mkuu kwa kiwango cha juu.

Bwana Obama amesema dola bilioni 700 za mipango ya kuunusuru uchumi wa Marekani ni hukumu ya mwisho kwa utawala wa chama cha Republican.

Amesema Bwana McCain alikuwa amekosea katika suala la Iraq na amemfananisha na Rais Bush. Mgombea wa chama cha Republican Seneta Mac Cain amemuelezea mpinzani wake hana uzoefu wa kuongoza.

Katika mdahalo huo hakuna aliyemuangusha mwenzake, ila maoni ya awali yanaonesha Bwana Obama amefanya vyema zaidi.

Si Kila Kiongozi ni Fisadi - JK


RAIS Jakaya Mrisho Kikwete amesema si kila kiongozi wala kila mtumishi wa umma barani Afrika ni mla rushwa ingawa amekiri kwa kiasi fulani tatizo hilo bado lipo barani humo. 

Rais alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu maswali baada ya kumaliza hotuba yake kwenye mkutano na wajumbe wa taasisi ya Foreign Policy Brain Trust ambayo ni ya wabunge wenye asili ya Afrika mjini Washington. 

"Tusijiweke katika hali ya kutengeneza mazingira ya kwamba kila jambo linaloendelea katika Afrika ni rushwa tu," alisema Rais Kikwete. 

Aliongeza kuwa: "Hatukatai kuwa ipo rushwa katika Afrika. Tunachosema ni kwamba jambo hilo linatiwa chumvi nyingi kupita kiasi". 

Kuhusu Tanzania, Rais Kikwete alisema kuwa Serikali yake inapambana kwa dhati na changamoto hiyo ya rushwa kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya Tanzania. 

"Moja ya dalili za Serikali inayokula rushwa ni kushuka kwa mapato ya Serikali au Serikali kushindwa kukusanya mapato. Mapato yetu (Tanzania) yamekuwa yakiongezeka kila mwaka tokea tulipoingia madarakani," alisema Rais Kikwete na kushangiliwa.

Atimaye Serikali Yalainika Kwa NMB

BAADA ya serikali kupiga chenga tangu Agosti 28 kusaini mkataba wa malipo ya mkupuo na maslahi mengine, serikali jana ilisalimu amri kwa wafanyakazi wa benki ya NMB iliposaini mkataba huo, lakini shughuli ya kusaini ikiwa imetanguliwa na mvutano mkubwa.

Uamuzi wa kusaini umefikiwa na serikali baada ya wafanyakazi hao kugoma kwa siku mbili na kusababisha adha kubwa kwa wateja wa benki hiyo, wengi wakiwa wafanyakazi wa serikali, wakiwemo wa taasisi nyeti kama jesi, Polisi na halmashauri.

Kipengele hicho kinaeleza kuwa hisa za wafanyakazi zitakuwa zinasimamiwa na hazina badala ya makubaliano ya awali kuwa hisa hizo zisimamiwe na wafanyakazi wenyewe kupitia Tuico-chama cha wafanyakazi wa viwandani na taasisi za fedha.

“Msiturudishe nyuma... haya mambo tulishayajadili siku nyingi chini ya wanasheria na tukakubaliana na kilichotuleta hapa leo ni kutiliana saini tu, si kuendelea kujadili suala hili,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.

“Hatukitaki kipengele hicho kiondolewa kwanza kwa sababu mwanzo hakikuwepo mmekiingiza kiujanja ujanja na ndiyo maana mmeleta mkataba huu dakika za mwisho. Sasa msimamo wetu ni kwamba hatukitaki la sivyo hatusaini.”

Kifo Cha Wangwe Chageuka Dili Kampeni za Tarime

MAMBO yanayojitokeza katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Tarime yanazidi kuvuruga amani na utulivu yakionyesha wazi kuwa kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Chacha Wangwe ni mtaji mkubwa wa kisiasa.

Tangu kufariki dunia kwa mwanasiasa huyo machanchari katika ajali ya gari katika eneo la Pandambili, wakati akitoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam, mambo mengi yamekuwa yakijitokeza katika sura ya kutaka kukitumia kifo hicho kama ngazi ya kupandia kisiasa na na kujiongezea umaarufu wa kushinda jimbo hilo.

Dalili za kwanza kabisa za kutumia msiba huo kama mtaji, zilijionyesha katika kampeni za mgombea wa CCM, ambapo mmoja wa ndugu wa marehemu Wangwe alisimama kwenye jukwaa na kutoa tuhuma za wazi za kukihusisha kifo cha ndugu yake na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Katika hali inayodhihirisha kuwa kifo hicho kishikiwa kidedea kuwavusha watu kisiasa, hata vyama vingine, kikiwamo cha Demokratic Party cha Mchungaji Chritopher Mtikila vimeanza kutumia agenda ya kifo cha Wangwe kama panga la kuwakata makali Chadema.

Watoto Afrika Wakutana Dar


Watoto kutoka nchi tisa za Afrika wako Dar es Salaam kuhudhuria mkutano kwa ajili yao juu ya changamoto wanazopata watoto wanaoishi katika mazingira magumu na ukubwa wa tatizo la Ukimwi. 

Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Dk Fatma Mrisho, alisema Dar es Salaam jana kuwa hisia, mitazamo na mahitaji ya watoto wa Afrika vitawasilishwa kwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) Rais Jakaya Kikwete atakayewahutubia watoto hao kesho. 

“Watoto wana tatizo la kipekee lakini lazima tukae tuone kuna haja ya kuboresha mtazamo wetu,” alisema Dk Mrisho na kueleza kuwa huenda tatizo la Ukimwi kwa watoto lina sura tofauti na ile inayofahamika katika jamii. 

Mmoja wa watoto wanaoiwakilisha Tanzania katika mkutano huo siku mbili, Nyabuchwenza Methuseka alisema, jamii inapaswa kuwajali watoto wanaoishi katika mazingira magumu ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wapate elimu. Mwezeshaji Mkuu wa mkutano huo, Richard Mabala alisema, watoto wanaohudhuria wanatoka Burundi, Lesotho, Malawi, Msumbiji, Afrika Kusini, Ethiopia, Zambia, Kenya, na wenyeji Tanzania.

Tenga Bado Kukata Shauri


RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Leodegar Tenga ameshindwa kuweka bayana azma yake kama atawania tena nafasi hiyo au la kwenye uchaguzi ujao unaotarajia kufanyika Desemba.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Tenga alisema kuwa ni mapema sana kuzungumzia suala hilo kwa vile bado kuna miezi mitatu kabla ya kufanyika uchaguzi huo.

Alisema yeye analojua ni kwamba uchaguzi upo palepale na utafanyika kwa mujibu wa katiba ya shirikisho hilo.

''Niwahakikishie tu kwamba uchaguzi upo pale pale na utafanyika kama katiba yetu inavyojieleza,'' alisema Tenga.

Alisema kuwa endapo atazangumzia suala hilo kwa wakati huu itazusha mijadala miongoni mwa wadau wa mpira hapa nchini na kusahau kujadili mambo muhimu ya kutekeleza programu ya maendeleo.

''Miezi mitatu ni mingi sana siwezi kuweka bayana kama nitaomba nafasi au la kwani kwa kufanya hivyo tutasababisha tuweke pembeni masuala ya maendeleo ya soka na kujadili uchaguzi,'' alisema Tenga.

Tenga alisema kuwa jambo la muhimu ambalo linapaswa kujadiliwa na wadau wa soka hapa nchini ni kufanya tathimini ya ni kipi kimefanyika katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake na kupanga mikakati ya siku zijazo.

Aliongeza kuwa TFF ni si mali ya watu wachache bali ni mali ya watu wote hivyo kwa wakati huu sera ya uongozi wake ni kufanya kazi kulingana na utashi wa wadau wa soka ili kupiga hatua ya maendeleo .

Saturday, September 27, 2008

katuni Leo

Pinda, Odinga Wazungumiza Serikali za Mseto Afrika


Serikali za Kenya na Tanzania zimesema uundwaji wa serikali za mseto barani Afrika si utaratibu wa kudumu na kuna haja ya kuwapo kwa demokrasia ya kweli, inayotoa haki kwa pande zote zinazoshiriki kwenye uchaguzi. 

Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga alisema Dar es Salaam jana kuwa, bara la Afrika lipo katika kipindi cha mpito cha kujiondoa katika mfumo wa udikteta, chama kimoja na tawala za kijeshi. Odinga aliyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliomshirikisha yeye na mwenyeji wake, Waziri Mkuu Mizengo Pinda. 

Alisema, maendeleo ya demokrasia yanatofautiana baina ya nchi na nchi, hivyo wao wanaamini yaliyotokea Kenya na Zimbabwe si mfumo wa kudumu katika siasa za Afrika. “Sisi tulifunga bao lakini refarii akasema eti ni offside, na Grigila naye akasema eti hakujua nani kafunga,” alisema Odinga ili kuonyesha upungufu uliopo kwenye uendeshaji wa uchaguzi Afrika na akadai hata Rais Robert Mugabe alicheza mpira peke yake akasema amefunga bao. 

Waziri Mkuu Pinda alisema ipo haja ya kuwa na mfumo unaotoa haki kwa pande zote na kwamba, wakati mwingine serikali za mseto zinatokana na mazingira ya maeneo husika hasa kuokoa maisha ya wananchi. Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Waziri wa Nishati wa Kenya, Kiraitu Murungi, na Waziri wa Elimu ya Juu wa nchi hiyo, Dk. Sally Kosgei, Waziri Pinda alitoa mfano wa Kenya kwamba, kama upande mmoja ungeendelea kung’ang’ania madaraka, Wakenya wangeendelea kuuana. 

Zikiwa Zimebaki Siku 38, Obama na McCain Watoana Jasho Kwenye Mdahalo


Katika Mdahalo wao wa kwanza kuonyeshwa kwenye TV, Sen. John McCain amemsema Sen. Barack Obama kuwa ni mtu ambaye hana uelewa katika mambo ya msingi, huku Sen. Obama akimfananisha mambo yake McCain na rais wa sasa Bush.

"I'm afraid Sen. Obama doesn't understand the difference between a tactic and a strategy," McCain said as the two traded jabs over Iraq.

Obama shot back, "I absolutely understand the difference between tactics and strategy. And the strategic question that the president has to ask is not whether or not we are employing a particular approach in the country once we have made the decision to be there."

McCain drew from his experience overseas as he tried to portray himself as the more qualified candidate.

"Incredibly, incredibly Sen. Obama didn't go to Iraq for 900 days and never asked for a meeting with Gen. [David] Petraeus," he said. 



Mke Wa Wangwe Ataka Tume Iundwe


MJANE wa aliyekuwa mbunge wa Tarime, marehemu Chacha Wangwe, Mariam Zakayo Wangwe amemtaka Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta, kuunda tume huru kuchunguza kifo cha mumewe kutokana na kutoridhishwa na uchunguzi wa polisi kuhusisha suala hilo na kosa la usalama barabarani.

Mbali na kumtaka Spika kufanya hivyo pia ameiomba serikali ifanye juu chini kuwasaidia katika uchunguzi wa kifo cha Wangwe.

“Sipendi mambo haya yaishe hivi hivi na familia ya Wangwe hatujaridhishwa na namna polisi wanavyofuatilia kifo cha Wangwe kwa kuwa sina imani na polisi,” alisema Mariam.

Alisema kuwa kama polisi wanadai kuwa kifo cha Wangwe kimetokana na kosa la usalama barabarani basi hakuna haja ya Deus Mallya kuwekwa ndani.

Alisema ana wasiwasi na uchunguzi unaofanywa na polisi kwani hawajawahi hata kufika kumuuliza kuhusu kifo cha Wangwe akiwa kama mke wake.

“Hawajawahi kufika kutaka maelezo yangu labda ningewasaidia kwa kiasi fulani, katika maelezo ya Deus kuwa alikuwa amelala na Wangwe kukutwa kiti cha abiria basi atafutwe mtu wa tatu ambaye alikuwa akiendesha gari hilo,” alisema Mariam.

Alioneza, “Upelelezi ufanyike zaidi kwani hakijafanyika chochote hadi hivi sasa ajali ni ya ajabu na kama polisi wanasema ni kosa la usalama barabarani basi Deus Mallya aachiwe huru,”

Alioneza, “Upelelezi ufanyike zaidi kwani hakijafanyika chochote hadi hivi sasa ajali ni ya ajabu na kama polisi wanasema ni kosa la usalama barabarani basi Deus Mallya aachiwe huru,”

Alidai kuwa aina ya kifo cha Wangwe kilivyotokea ni mambo yanayotokea Kenya hivyo huenda waliosababisha kifo hicho wametokea Kenya.

“Namna ajali ilivyotokea ni kama vile mambo yanavyotokea Kenya,” alisema.

Akizungumzia kuhusu hali ya mumewe mwezi mmoja kabla ya kifo chake Mariam alisema hali ilikuwa mbaya nyumbani kwake kutokana na Wangwe kuwa katika pilika pilika nyingi hasa baada ya kuenguliwa umakamu mwenyekiti wa Chadema.

Alisema, “Maisha ya Wangwe yalikuwa ya misukosuko sana dakika za mwisho”.

Kuhusu Chadema Mariam amekilaumu chama hicho kwa kutowajali tangu Wangwe afariki na kudai kuwa wanaweza wakawa wanahusika na kifo hicho kwani chuki yao kwa Wangwe wameipeleka mpaka kwa watoto.


Friday, September 26, 2008

Kikwete Ateta na Bill Gates

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Kikwete (kushoto) akizungumza na Bw. Bill Gates ambaye ni Mwenyekiti wa Bill na Melinda Gates Foundation jijini New York, Marekani jana

Zombe Wamtosa


MKUU wa Upelelezi wa kesi inayomkabili aliyekuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi, Abdallah Zombe na wenzake 12, ameieleza Mahakama Kuu kuwa karibu watuhumiwa wote walipotakiwa kuandika maelezo yao kwa mara ya pili, walimgeuka Zombe. 
Askari wasiokwenda msitu wa Pande walikuwa watatu ambapo mmoja kati yao shahidi huyo alidai hamkumbuki. 

Akihojiwa na Wakili wa utetezi, Majura Magafu mbele ya Jaji Kiongozi, Salum Massati, Mkumbi ambaye ni shahidi wa 36, alidai watu hao walikamatwa Sinza Palestina Block C kwa utaratibu bila mashambulizi na kwenda kuuawa katika msitu huo. Pia hawakuwa majambazi na hawajahusika na wizi wa kampuni ya Bidco. 

“Wao waliungana na wenzao na kudanganya katika maelezo yao kuwa waliouawa walikuwa majambazi na waliiba Bidco wakati si sahihi,” alidai. Hata hivyo, Jaji Massati alipomhoji shahidi kwa namna gani askari wadogo walihusika katika tukio hilo wangewezaje kuzuia matukio ya Sinza na katika Msitu wa Pande yasitokee, Mkumbi alijibu “walitakiwa baada ya kutoka katika msitu wa Pande immediately (haraka) waripoti tukio hilo kwa ofisa yeyote wa polisi.” 

Sehemu ya mahojiano kati ya wakili Magafu na shahidi huyo wa 36 ambaye ni Mpelelezi Mkuu katika kesi inayomkabili Zombe na wenzake 12, Sydney Mkumbi yalikuwa kama ifuatavyo: 

Wakili: Unafahamu washitakiwa wanakabiliwa na nini? 

Shahidi: Nafahamu, kosa la mauaji Wakili: Wapi? Wakili: Katika Msitu wa Pande uliopo Mbezi Luisi. 

Wakili: Zombe alikuwapo? Shahidi: Hakwenda msituni. Wakili: Zombe alikuwapo Sinza wakati marehemu wanakamatwa? Shahidi: Hakuwapo. Wakili: Imedaiwa kulikuwepo mapambano kati ya marehemu na askari katika ukuta wa Posta huko Sinza, je, Zombe alikuwepo? Shahidi: Kwenye mapambano hakuwepo. 

Wakili: Ukiachilia mbali maelezo ya Rashidi kuwa Zombe aliwasiliana na mshitakiwa wa pili yaani Christopher Bageni, kuna sehemu Zombe amehusishwa? Shahidi: Mshtakiwa namba mbili aliandika barua kwa DCI akitaka Tibaigana awepo. Wakili: Unayo? 

Shahidi: Sina hapa? Wakili: Jana hukusema. Shahidi: Ningeulizwa ningesema. Wakili: Umezua leo asubuhi hii. Shahidi: Wewe ndiyo umezua? Wakili: Katika upelelezi wako, kuna sehemu uligundua watuhumiwa walikaa pamoja wakasuka njama za kuwaua hao marehemu? Shahidi: Kwa mtiririko ulivyo walikuwa pamoja, walikutana Block C na wakasema ‘tumeamriwa tukachinje’ 

Wakili: Waliwasiliana? Shahidi: Ndiyo kwa simu ya upepo na mawasiliano ya simu ya mkononi. 

Wakili: Unazifahamu simu za Zombe na Bageni? Shahidi: Nilikuwa nazijua lakini sasa sizijui tena. Wakili: Ulienda kufuatilia mazungumzo yao katika ofisi za simu? Shahidi: Nilifanya hivyo, niliagiza kwa maneno Wakili: Ulipata majibu? 

Shahidi: Nilipata majibu kuwa muda ulishapita kwani Vodacom wanatunza maongezi kwa miezi sita halafu wana destroy. Wakili: Kuua ni amri halali? 

Shahidi: Si amri halali. Wakili: Nikiwa na bosi wangu nikamuona anaiba nami ntakuwa nimefanya kosa? Shahidi: Utawajibika, kwa nini usizuie wizi usitendeke? 

Wakili: Akiwa na silaha mimi sina je? Shahidi: Ungetakiwa uripoti ofisa fulani ametenda kosa ukinyamaza unahusika. Wakili: Kuna malalamiko askari walichukua pesa za marehemu. 

Shahidi: Nilisikia, lakini hilo ni kosa la wizi Wakili: Mtu anaweza kuuawa pasipo sababu? Shahidi: Inawezekana. Wakili: Swali langu la msingi sasa linasema ili uweze kumwua mtu lazima uwe na chuki naye kama si bahati mbaya? Shahidi: Lazima sababu iwepo. 

Wakili: Washtakiwa walikuwa wakifahamiana na marehemu? Shahidi: Hawafahamiani. Wakili: Unakubaliana nami kama si tukio la Bidco wasingekutana? 

Shahidi: Ni kweli. Wakili: Katibu wa Tume ya Kipenka alikuambia washtakiwa walipora pesa? Shahidi: Sikumhoji. 

Wakili: Hapa mahakamani imedaiwa sababu ya wale kuuawa ni askari walipora pesa, ulifahamu? Shahidi: Nilifahamu baadaye. Wakili: Hadi sasa hufahamu? 

Shahidi: Nafahamu kwa sababu ya ushahidi wa kina Lunje Wakili: Si mliwapandikiza? Shahidi: Nafsi iliwasuta. Wakili: Mlipewa kazi nzuri, lakini mlikuwa biased Shahidi: Uliza swali Wakili: Uliwahi kumuuliza Bageni begi la pesa lilikwenda wapi? Shahidi: Sikumhoji. 

Wakili: Rashidi na Rajabu hawakuwa wakweli, unasemaje? Shahidi: Walikuwepo katika tukio, hawakukiri kuua walishuhudia mauaji. Wakili: Nani mashahidi? 

Shahidi: Wote waliamriwa kuandika maelezo yao upya, walifuatwa rumande na karibu wote isipokuwa mshitakiwa wa kwanza (Zombe) waliandika maelezo yanayofanana na Rashidi na Rajabu. Wakili: Rashidi alisema walipewa kikaratasi, ni kweli? 

Shahidi: Ndiyo alipewa na akasema ‘hata mke wangu simuachii, ntakuwa nacho mwenyewe’ 

Wakili: Kilikuwa na saini ya mkubwa? Shahidi: Alinionyesha tu na sikuona saini Wakili: Ni mwandiko wa mtu au typing? Shahidi: Kiliandikwa kwa typewriter . Baada ya kuhojiwa na Magafu, 

Mkumbi alihojiwa na wakili Longino Myovela na mahojiano yao yalikuwa kama ifuatavyo: Wakili: Kama mpelelezi unaamini Koplo Saad aliua? Shahidi: Naamini 

Wakili: Ungekuwa katika Tume ungewaingiza hawa wengine (watuhumiwa 12) wakati Saad ndo ameua? 

Shahidi: Uchunguzi ungeniongoza. Wakili: Kuwakamata marehemu ni kosa? Shahidi: Si kosa wanatekeleza kazi ya polisi. 

Wakili: Ni lazima junior polisi atekeleze amri ya wakubwa? Shahidi: Ni sahihi kutekeleza amri ya kiongozi Wakili: Kwenda msitu wa Pande kwa amri ni sawa? 

Shahidi: Ni amri halali kwenda msitu wa Pande, lakini utekelezaji wake si halali. Wakili: Zaidi ya kuona Saad akiua, Rashid alikuambia nini? Shahidi: Rashidi alisema Bageni alikuwa anawasiliana kwa simu na kiongozi wake kwa sababu alikuwa akisema ‘afande afande’.

Motlanthe Awa Rais wa Mpito Bondeni


Naibu kiongozi wa chama tawala cha African National Congress cha Afrika Kusini Kgalema Motlanthe ameapishwa kuwa rais wa muda nchini humo.

Bwana Motlanthe anachukua nafasi ya Bwana Thabo Mbeki aliyejiuzulu wiki iliyopita baada ya chama chake mwenyewe kusisitiza afanye hivyo.

Bw Montlanthe ameshinda robo tatu ya kura za siri zilizopigwa katika bunge la nchi hiyo mjini Cape Town.

Hata hivyo kulikuwa na zaidi ya kura arobaini zilizoharibika.

Trevor Manuel ambaye ni waziri wa afya anayeheshimika sana nchini humo ameshikilia nafasi yake licha ya kutaka kuachia ngazi.

Kujiuzulu kwa Bw Mbeki kulisababisha mawaziri wengi wa nchi hiyo kujiuzulu.

Bw Manuel alikuwa ni mmoja kati ya wawakilishi 11 wa bunge hilo kujiuzulu lakini amesema ameridhika kumtumikia rais mpya.

Mothlante alichukua nafasi ya naibu rais wa chama tawala cha ANC mwaka jana akiungwa mkono na Jacob Zuma.

Bw Zuma ambaye ndiye kiongozi wa chama hicho anatarajiwa kuwa rais wa nchi hiyo katika uchaguzi unaofanyika mwakani.

Mtikila Apata Kipigo

Mchungaji Christopher Mtikila baada ya kushonwa nyuzi kisogoni kutokana na jeraha la jiwe akiangalia shati lake lililolowa damu baada kupata matibabu mjini Tarime, Alhamisi katika kampeni za kisiasa.

Thursday, September 25, 2008

Katuni Leo

Mgao Wa Umeme Warudi Tena

Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), limetangaza mgao wa umeme kwa kipindi kisichojulikana. Hatua hiyo imeelezwa kuwa inafuatia kuharibika ghafla kwa mashine tatu za kuzalisha nishati hiyo kwenye kituo cha Songas. 

Taarifa fupi iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana jioni na Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud, ilieleza kwamba, kuharibika kwa mashine hizo kumesababisha upungufu wa megawati 110. 

Taarifa hiyo iIisema upungufu huo ni sawa na asilimia 16 ya kiwango cha mahitaji ya umeme nchini. 

``Shirika limejitahidi kadiri ya uwezo wake kujaza pengo hilo la uzalishaji kwa kutumia mitambo mingine ya gesi asilia na ile ya kutumia maji, lakini bado kutabakia na upungufu wa umeme na kulazimu kufanyika mgao wa umeme wa kiwango cha megawati 40 kuanzia saa 12:00 jioni hadi saa 5:00 usiku,`` alisema Badra katika taarifa hiyo. 

Kwa mujibu wa meneja huyo, mgao ulianza jana jioni sehemu mbalimbali nchini isipokuwa jijini Dar es Salaam. 
Aidha, alisema taarifa zaidi kuhusiana na maeneo yatakayohusika na mgao huo zitatolewa leo.

Wanamgambo wapigwa na jeshi Nigeria


Kundi kuu la wanamgambo wanaopigania mafuta nchini Nigeria limeshutumu jeshi la nchi hiyo kwa kufanya mashambulio ya anga dhidi ya washirika wao.

Movement for the Emancipation of the Niger Delta (Mend), lilitangaza kusitisha mapigano siku tatu zilizopita.Msemaji wa jeshi la Nigeria ameeleza kuwa hana taarifa zozote za mashambulio ya anga kufanyika Jumanne.

Mend limesema lisingependa kutumbukizwa katika mapigano na kuhatarisha mpango wa amani, limedai kuwa litaendelea kutekeleza mpango wa kusitisha mapigano.

Makundi kama Mend yanadai kuwa yanapigani udhibiti wa utajiri wa mafuta kwenye jimbo la Niger Delta ambalo watu wake ni mafukara, lakini kundi hilo linatuhumiwa kwa kujipatia fedha nyingi kutokana na biashara haramu ya mafuta ya wizi.

Walinda amani washambuliwa Somalia


Mapigano mapya yamezuka Mogadishu mji mkuu wa Somalia, huku majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Afrika yakishambuliwa na wanamgambo wa kisomali.

Raia wasiopungua 15 wameuawa tangu mapigano yalipoanza siku ya Jumanne na idadi kubwa ya watu wamekuwa wakiukimbia mji huo.

Wanamgambo waliwashambuliwa walinda amani wa Umoja wa Afrika kutoka Uganda, ambao walijibu mashambulizi kwa vifaru na mizinga.

Siku ya Jumatatu, watu 30 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mojawapo ya mapigano makali zaidi kutokea Mogadishu kwa miezi kadhaa.

Wednesday, September 24, 2008

Katuni Leo

Watoto 90 Watekwa Uganda

Umoja wa mataifa umetoa wito kutaka kuchiliwa huru kwa watoto 90 wanaoshikiliwa na waasi wa Uganda kaskazini-mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Unicef imesema ina wasi wasi kuhusu watoto hao, waliotoroshwa kutoka katika shule mbili juma lililopita, kwamba watalamishwa kushiriki katika mapigano ya kivita.

Shirika hilo la kuhudumia watoto la Umoja wa mataifa limesema chifu wa kijiji kimoja pia alitekwa nyara na watu wengine watatu kuuawa.

Kundi la waasi wa LRA limekuwa likifanya maasi kwa zaidi ya miaka 20 ambapo zaidi ya watu milioni mbili wamekimbia makazi yao.

Unicef imesema watoto 50 walitoroshwa kutoka shule moja ya msingi huko Kiliwa na wengine 40 kutoka shule ya sekondari ya Duru katika uvamizi uliofanyika kwa mpigo ndani ya jimbo la Oriental.Pia kijiji kingine cha Nambia, kilishambuliwa.

NMB Yapewa Masaa 3 Tu!!

JAJI wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Jaji Mfawidhi Ernest Mwipopo, jana alibatilisha mgomo wa wafanyakazi wa Benki ya NMB na kuwataka warejee kazini ndani ya muda wa saa tatu, uamuzi ambao umeridhiwa na wafanyakazi.

Akitoa hukumu hiyo jana, Jaji Mwipopo alizitaka pande mbili zinazopingana kutoa matangazo kwenye vyombo vyote vya habari kuwajulisha wafanyakazi hao kuwa wanatakiwa kurejea kazini kuanzia saa 11:25 jioni jana hadi leo 2:00 asubuhi.

"Aya hizo zinagongana na nafasi ya serikali kwenye madai ambayo ni msingi wa ugomvi," alisema. "Aya ya kwanza imeitaja serikali kuwa ndio iliyogoma kusaini makubaliano. Kutokana na hali hiyo kuna uwezekano kuwa mgogoro huo umeelekezwa kwa NMB kwa sababu ndio taasisi pekee mnayoweza kuigomea."

Alisema hoja ya pili inayofanya mahakama isiutambue mgomo huo na kuuita haramu na batili, ni muda wa kutolewa kwa nositi ya kuanza kwake.

Alifafanua kuwa, notisi hiyo ya saa 48 iliyotolewa Ijumaa ilimaanisha kuwa mgomo huo ulitakiwa uanze saa 10:45 Jumapili, muda ambao saa hizo 48 ulikuwa unaisha. Lakini badala yake wafanyakazi walianza mgomo huo saa 2:00 asubuhi Jumatatu.

Hali kadhalika jaji huyo alifahamisha kuwa mgomo huo ulipaswa kuanza jana na sio juzi endapo notisi yake ingetolewa kwa kutumia siku za kazi badala ya saa kwani sheria ya kazi, haitambui siku za Jumamosi na Jumapili kuwa ni siku za kazi.

"Hoja ya pili ni timing (muda), kama notisi hiyo ni ya saa 48 na ilipokewa Ijumaa saa 10:45 jioni, muda wake ungeisha saa 10:45 Jumapili. Kwa nini hamkugoma siku hiyo na mkaamua kusubiri hadi Jumatatu?" alihoji Jaji Mwipopo na kuongeza:

"Lakini ikumbukwe kwamba, sura ya kwanza ya Sheria ya Kazi... haitambui Jumamosi na Jumapili kuwa ni siku za kazi, hivyo kuhesabu siku hizo kuwa siku za kazi sio sahihi."

Kwa mujibu wa Jaji Mwipopo ni jukumu la mahakama kutafsiri notisi ya saa 48 inaisha lini, kwa kuwa sheria haikutoa tafsiri kuhusu notisi ya masaa hasa endapo notisi hiyo inatolewa mwishoni mwa juma.

"Kutokana na mambo hayo, mahakama imetengua mgomo huo na kuutangaza kuwa ni haramu na batili hivyo hautakiwi kufuatwa. Kwa mujibu wa kifungu 84 cha sheria za ajira, naamuru ndani ya masaa matatu, kuanzia sasa, wafanyakazi wote warejee kazini," alisema Jaji Mwipopo na kuongeza:

"Nimeangalia kwa makini na kugundua udhaifu wa mambo matatu ambayo yanafanya mgomo huo uonekane batili na haramu, hivyo ninatoa amri na maagizo kuhusu suala hilo.

"Naamuru mfanyakazi ambaye hakuweza kuripoti kazini leo (jana) awe ameripoti kazini kwake kesho (leo) saa 2:00 asubuhi na naagiza uongozi wa NMB uwapokee wafanyakazi hao wote bila masharti na usiwape adhabu kwa kushiriki mgomo huo."

Baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwandani na Taasisi za Benki (Tuico), Boniphace Nkakatisi kuwaeleza uamuzi huo, waliweka msimamo kuwa wasingerejea kazini na kumpa kiongozi huyo wakati mgumu wa kuwaelewesha.

"Nina waomba mrudi kazini kwa moyo mkunjufu tena kwa kujituma kama awali na kutii amri ya mahakama wakati sisi tunarudi mezani kwa majadiliano zaidi," alisema Nkakatisi.

Hata hivyo, hoja ya Wakili Mbwambo ilipingwa na wakili wa wafanyakazi, Khamis aliyesema: "Mheshimiwa jaji, Mbwambo hakuwa mkweli na hataki kuwa muwazi. Kutaka wafanyakazi hao warejee kazini ni kuendeleza mgogoro. Njia mwafaka ni watu kukutana na kufikia mwafaka."

Kabla ya majibizano hayo, Jaji Mwipopo alitumia muda mwingi kuwauliza maswali mawakili hao na ifuatayo ni sehemu ya mahojiano yao:

Jaji: Kwa nini, msomi Khamis, mahakama isiamini kuwa mgomvi wa Tuico ni serikali iliyokataa kusaini mabaliano yenu na sio NMB?

Wakili Khamis: Ndio maana nilisema kuna haja ya sisi kupata muda wa kuwasilisha nyaraka zetu kwa maandishi kwani makubaliano yalihusu pande tatu, wafanyakazi, NMB na serikali. Kabla ya serikali, NMB ilitakiwa iwe imesaini kwanza.

Jaji: Baada ya kutoa notisi ya saa 48 Ijumaa saa 10:45 jioni, kwa nini msingegoma Jumapili siku ambayo notisi yenu iliisha badala yake mkachagua Jumatatu?

Wakili Khamis: Sheria inataka watu wagome baada ya notisi, na kwa mujibu wa sheria hiyo hakuna ubaya watu kugoma muda wowote baada ya muda wa notisi hiyo kumalizika.

Jaji: Kwa nini masaa hayo 48 hayakuwa ya siku za kazi na hivyo kuishia Jumatatu na mgomo mkaanza leo (jana)?

Wakili Khamis: Siku za kazi sio za tarehe za mwezi, ni siku ambazo wafanyakazi wa taasisi wanatakiwa kufanya kazi na kwa NMB ni siku zote kwani ATM zinafanya kazi masaa 24, hivyo ni sahihi kuhesabu Jumamosi na Jumapili kuwa ni siku za kazi kwa NMB.

Baada ya mahojiano na wakili wa wafanyakazi, Jaji Mwipopo alimgeukia wakili wa NMB na sehemu ya mahojiano yao ni kama ifuatavyo:

Jaji: Kwa nini nyie (NMB) msionekane pia kuwa mna hila na mnashirikiana na wafanyakazi hao kuishinikiza serikali isaini makubaliano kwa kutotoa taarifa mapema kwamba Jumatatu mgomo unaanza?

Wakili Mbwambo: Tunashukuru kwamba unatukumbusha uwezekano wa kuwasiliana na ofisi yako hata siku za mwisho wa juma, lakini katika hali ya kawaida isingeweza kuwaza kwamba tungeweza kukupata siku hiyo.

Jaji: Kwa nini mnaomba viongozi hawa wakamatwe, wafilisiwe na wafungwe kama wafungwa wa madai badala ya kuomba mahakama izuie mgomo?

Wakili Mbwambo: Hili ni ombi moja tu, kumbuka pia tumeiomba mahakama ichukue hatua nyingine yoyote inayoona inafaa kunusuru hali hiyo.

Baada ya maswali na majibu hayo yaliyodumu kwa takriban saa 1:30 Jaji Mwipopo alisema: "Kuhusu maombi ya NMB kwamba viongozi wakuu wanne wasikilizwe leo na amri itolewe ya kukamatwa, kufilisiwa na kufungwa kama wafungwa wa madai, natoa amri kwamba mahakama imewapa muda ili waweze kujitetea kwa maandishi na vielelezo na kuwasilisha pingamizi la kiapo kesho, (leo) kesho kutwa wampe nakala ya hati hiyo wakili wa mwajiri na Septemba 26 tukutane hapo saa 4:00 asubuhi kuendelea na shauri hili."

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda na Taasisi za Fedha nchini (TUICO) Boniphace Nkakatisi akiwa katika Divisheni ya Mahakama ya Kazi walipofikiswa jana kujibu mashitaka ya kuongoza mgomo wa wafanyakazi wa Benki ya NMB.

Tani 34,000 Za Maziwa Zakamatwa


MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA), imekamata na kuzuia zaidi ya tani 34,000 za maziwa ya unga zilizoingizwa nchini hivi karibuni kutoka China.

Kukamatwa kwa maziwa hayo kunafuatia ukaguzi unaoendelea nchini baada ya maziwa yanayotengenezwa China kusababisha vifo vya watoto na kusababisha nchi nyingi duniani kupiga marufuku uagizaji wa maziwa hayo.

Katika msako huo, TFDA imebaini kuwepo mifuko 1629 (sawa na tani 34) ya maziwa ya unga toka China .

Mkurugenzi wa Usalama na Chakula wa TFDA, Raymond Wigege aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa maziwa hayo yalikamatwa mwishoni mwa wiki baada ya kuingizwa nchini siku chache tangu mamlaka hiyo isitishe kutoa vibali vya uagizaji na usambazaji wa maziwa na bidhaa zenye viambata vya maziwa kutoka China.

Alisema maziwa hayo yamezuiliwa kwa mujibu wa sheria wakati uchunguzi zaidi unafanyika ili kubaini kama maziwa hayo yaliyoingizwa yana athari yoyote kwa binadamu au la.

Hivi karibuni TFDA ilitoa taarifa ya kusitisha kutoa vibali vya uagizaji na usambazaji wa maziwa na bidhaa zenye viambata vya maziwa kutoka nchini China baada ya habari kutoka Mamlaka za Udhibiti wa Usalama wa Chakula wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kueleza kuwa bidhaa hizo zina athari kwa binadamu.

Imeelzwa kuwa maziwa hayo au viambata vyake vina sumu aina ya melanmine ambayo huathiri figo kwa watoto.

Hadi kufikia jana watoto zaidi ya watoto 1000 wenye umri wa chini ya mwaka mmoja waliugua kutokana na kula vyakula hivyo na wanne kati yao wamepoteza maisha.

Mawaziri 10 Waondoka Na Mbeki


Mawaziri 10 katika serikali ya Afrika Kusini wamejiuzulu, hatua hiyo inatokana na kung'olewa madarakani kwa rais Thabo Mbeki na chama tawala cha African National Congress.

Miongoni mwao ni waziri wa fedha, Trevor Manuel anayesifika kwa kuimarisha uchumi wa nchi hiyo.

Wengine ni mawaziri wa ulinzi, usalama na ujasiriamali wa umma.Barua zao za kujiuzulu zimeidhinishwa na Bw Mbeki mwenyewe ambaye bado hajaondoka rasmi madarakani.

Kujiuzulu kwa makamu wa rais Bi Phumzile Mlambo-Ngcuka kulitangazwa mapema, naye akichukua hatua hiyo kumfuata rais Thabo Mbeki.

Kiongozi huyo aliyeng'olewa na chama chake hata hivyo amenukuliwa akisema atafungua kesi kupinga uamuzi wa mahakama kwamba aliingilia kesi dhidi ya Jacob Zuma.

Nini Kilimsibu Latoya


MWAKILISHI wa shindano la Big Brother Africa BBA 3 Latoya Lyakurwa amerudi nchini akitokea Afrika Kusini huku akisema yaliyotokea kwenye jumba hilo ni mchezo. 

Latoya aliwasili jana saa nane mchana akiwa na sura ya tabasamu na kuwaomba msamaha Watanzania wote kwa namna moja au nyingine na kuwachosha wakati alipokuwa kwenye shindano hilo. 

“Kutolewa kwangu siyo tatizo kubwa sana kwani kukaa kwenye jumba lile ni sawa na mtu ambaye yuko jela hakuna raha kabisa mle ndani kwani kila mtu anahitaji kuishi maisha ya uhuru kama hivi nilivyo sasa sawa nimeumia lakini nimefurahi kutoka pia” anasema. 

Alilalamikia kitendo cha kutoonyeshwa akiwa anafanya mambo mazuri zaidi ya yale ambayo yalikuwa hayafurahishi. 

Aidha, alisema kuwa alishtuka sana na kupata wakati mgumu pale alipoamriwa na Biggie kuwa anatakiwa kwenda kwenye chumba kichafu ‘Dampo” lakini alilazimika kukubaliana na hali hiyo. 

Latoya alisema kuwa anahisi mshindi wa shindano hilo kwa mwaka huu atatoka Angola ambapo wanawakilishwa na Ricco. 
Latoya ambaye ni mhitimu wa kidato cha sita anasema malengo yake ya baadaye ni kurudi tena shuleni na kuishi katika maisha yake ya kawaida. 

Wakati huohuo aliyekuwa mshiriki wa BBA2 Tatiana Dos Darego ambaye hivi sasa ni Balozi wa Matende na Mabusha aliwasili jana kwa mwaliko wa Unicef amemtaka Latoya kujituma ili kupata mafanikio. 

Latoya amekuwa mshiriki wa kwanza kutolewa kwenye shindano hilo ambako alidumu kwa takribani majuma manne.

Tuesday, September 23, 2008

Stooooop!!!


Baadhi ya wateja wa Benki ya NMB wakiwa nje ya tawi la Benki hiyo la Bank House lililopo mtaa wa Samora jana baada ya wafanyakazi wake kuwa katika kuanza mgomo jana wa kushinikiza maslahi zaidi kwa wafanyakazi.

Monday, September 22, 2008

Jamani Ntaenda Wapi Mimi!!!


Mkazi wa jijini Dar es Salaam akilia baada ya nyumba yao kubomolewa, kazi ya kubomoa nyumba inaendelea huku familia sita zikiwa zimekosa sehemu ya kuishi baada ya watu wanaodai kununua nyumba ya urithi ya watoto zaidi ya 10 wa marehemu, Yussuf Mbonde iliyopo Magomeni Mwembechai, kubomoa nyumba hiyo kwa kutumia greda huku wakilindwa na vijana wa kukodi maarufu kama mabaunsa pamoja na usimamizi wa polisi waliokuwa na silaha.

ANC Kupendekeza Rais wa Mpito


Chama Tawala nchini Afrika ya Kusini, kimesema kinatarajia kutoa jina la Rais wa mpito baadae leo, baada ya chama hicho kumlamzimisha Thabo Meki kujiuzulu.

Baleka Mbete ambaye ni spika wa nchi hiyo, ana nafasi kubwa katika chama hicho kupata nafasi ya kuwa rais wa mpito mpaka hapo mwakani kutakapo fanyka uchaguzi mkuu.

ANC kinamshinikiza Bw. Mbeki kujiuzulu kutokana na kile kinachosemekana kuwa alikuwa akishinikiza Bw. Zuma kuhukumiwa kutokana na kesi ya ufisadi iliyokuwa ikimuandama. Lakini jaji mmoja wa nchini humo aliifutilia mbali kesi ya Bw. Zuma na kusema huenda kulikuwa na maswala ya kisiasa katika kesi hiyo. Bw. Mbeki amekana shutuma hizo na kusema anaheshimu uamuzi wa chama cha ANC.

Sunday, September 21, 2008

Chakula Afrika Mashariki Mgogoro


Umoja wa Mataifa umesema takriban watu milioni 17 katika pembe ya Afrika wanahitaji chakula cha dharura na misaada mengine mara mbili ya ilivyotakiwa hapo awali.

Umoja huo umesema kiasi cha dola za kimarekani milioni 700 zinahitajika kwa ajili ya msaada huo wa dharura ili kuzuia hali hiyo isiongezeke.

Afisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu, John Holmes, amesema akiba ya chakula imepungua sana katika maeneo ya Ethiopia, Somalia, Eritrea, Uganda na kaskazini mwa Kenya.

Maeneo hayo yameathirika sana na ukame, migogoro na kupanda kwa bei za vyakula.

Bw Holmes amesema, " Huku hali ya ukame ikiongezeka na msimu wa njaa ukiendelea" idadi ya watu watakaoathirika inaweza kuongezeka.

Inakadiriwa kuhitajika jumla ya bilioni za kimarekani 1.4 ili kusaidia watu wanaohitaji msaada kwa mwaka huu peke yake.

Bw Holmes amesema takriban nusu ya idadi hiyo imepatikana lakini kuna upungufu wa dola za kimarekani milioni 716.